Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila uliowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari na Viongozi wa Jiji la Dar es Salaam kujadili hatua na mikakati ya pamoja kuimarisha usafi wa Mazingira katika Jiji la Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni Utekelezaji wa wito wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia kauli yake kuhusu
hali ya uchafuzi wa Mazingira katika Jiji la Dar es Salaam.
Amesema watanzania wote kwa kila kaya wanapaswa kuwa na
vifaa vya kutunzia taka (Dustins) angalau viwili au zaidi ili kurahisisha
utenganishaji taka, pia magari kuwa na kifaa kimoja, pamoja na kuwepo kwa mapipa katika stendi na
maeneo mbalimbali ya huduma huku akieleza umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa
vya usafi na vya kuwekea taka katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha shughuli
za usafi kufanyika kwa ufanisi.
Aidha Mhe. Chalamila amesema tayari Serikali imeanza mashirikiano na Taasisi za kifedha zikiwemo Benki na Kampuni za kuzalisha vifaa vya kutunzia taka ili kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa wingi huku akisisitiza kuwa mkakati wa kusafisha Jiji la Dar es Salaam hautegemei tu kuondoa taka bali kuchakata taka na kuzibadili kuwa bidhaa ikiwemo Gesi.
Pamoja na mikakati iliyojadiliwa, Mhe. Albert Chalamila
ametoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya Mvua za El ñino
zinazotarajiwa kunyesha ikiwa ni pamoja na kuzingatia ushauri na taarifa
zinazotolewa na Mamlaka husika.
Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe
akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema kila mwananchi ana haki ya kuishi katika mazingira safi na salama kwa
mujibu wa Sheria hivyo ni wajibu kwa kila mmoja kutunza na kuhifadhi
mazingira huku akisisitiza kuwa usafi wa
Jiji la Dar es Salaam unahitaji ushiriki na hatua za pamoja kutoka kwa
viongozi, vyombo vya habari na jamii ili kurejesha usafi wa jiji.





.jpeg)


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni