Nyumbani

NEMC YAPIGA KAMBI SABASABA – YAWAKARIBISHA WANANCHI KUPATA ELIMU YA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilipiga kambi viwanja vya sabasaba maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ili kutoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa wananchi waliotembelea banda hilo katika Jengo la Karume.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mhandisi Mwandamizi wa NEMC, Bw. Haji Kiselu, alisema Baraza limejipanga kikamilifu kuhakikisha elimu ya mazingira iliyo jumuishi inamfikia kila mwananchi, ili kwa pamoja tuweze kuyasimamia kwa maendeleo endelevu nchini.

Kwa upande wake, Mhandisi wa NEMC, Bw. Peres Ntinginya, alipozungumza, alisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja hivyo yapasa kuwajibika na kutoa  wito kwa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa matumizi yake husaidia kulinda afya ya binadamu na viumbe hai, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, pamoja na kuhifadhi mazingira kwa ujumla.

Naye Mkazi wa Rufiji, Bw. Ayubu Njanja, alisema elimu aliyoipata kutoka kwa Maafisa wa Baraza imempa mwongozo sahihi wa kuzingatia katika kuhakikisha 

Bw. Ayubu Njanja akipatiwa elimu ya mazingira kutoka kwa wataalam wakati wa msimu wa maonesho ya 49 ya Sabasaba. 




Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika  maonesho ya 49 ya Sabasaba 2025 




Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika  maonesho ya 49 ya Sabasaba 2025 


NEMC YATEKELEZA AGIZO LA RAIS, YAONGEZA HUDUMA VIWANJA VYA NZUGUNI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan la kuongeza muda wa kutoa huduma zake katika viwanja vya maonesho ya Nane Nane vilivyopo Nzuguni, Jijini Dodoma. 

Hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, hususan wakulima na wafugaji wanaoshiriki maonesho hayo, ili kuwajengea uelewa na kuwasaidia kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.

Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika maoneshoya wakulima, Nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma katika siku za nyongeza ikiwa ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza muda wa maonesho hayo

NEMC inaendelea kutoa elimu inayohusu masuala ya matumizi endelevu ya ardhi, uhifadhi wa vyanzo vya maji, na namna ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Vilevile, wananchi wameelimishwa kuhusu taratibu za kupata vibali vya mazingira na umuhimu wa kufanya Tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanzisha miradi.

Baraza hilo linaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake ili kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa. 

“Mazingira ni msingi wa maisha yetu. Tukiyaacha, na sisi tutapotea. Tushirikiane kuyatunza kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,”



Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika maonesho ya wakulima, Nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma katika siku za nyongeza ikiwa ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza muda wa maonesho hayo


NEMC YASHIRIKI HAFLA YA UFUNGAJI WA MAONESHO YA NANENANE, RAIS AONGEZA SIKU MBILI ZA KUTOA HUDUMA UWANJANI HAPO

Baraza la Taifa la Hifadhi na  Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu kwenye hafla ya ufungaji wa maonesho ya 32 ya wakulima (Nanenane) Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma leo

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo katika hotuba yake  amesisitiza umuhimu wa kilimo bora na endelevu kama mhimili wa maendeleo ya Taifa. 

Amesema sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi  ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, hivyo zinahitaji uwekezaji wa kutosha, ubunifu na usimamizi madhubuti ili kuijenga kesho bora kwa Watanzania wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiwasili katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma kufunga Maonesho ya Wakulima (Nanenane 2025) katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Ameelekeza Wizara ya Kilimo kuimarisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima, pamoja na kuunganisha nguvu katika kukuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan  ametangaza kuongeza siku mbili zaidi za maonesho hadi tarehe 10 Agosti ili kutoa nafasi kwa wananchi na wadau kuendelea kupata huduma na elimu mbalimbali.

" Maonesho haya ni siku nane, lakini kiuhalisia siku nane hazitimii kwani maandalizi yanachelewa, hivyo kuanzia mwaka ujao maandalizi ya maonesho yaanze tarehe 25/07." Ameelekeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan

Hafla hiyo ya ufungaji imehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu, Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Binafsi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya Wakulima (Nanenane 2025) katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Kwa upande wake, NEMC ilitumia maonesho haya kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira katika shughuli za kilimo na ufugaji, ikiwa ni pamoja na matumizi salama ya  mbolea, upandaji miti, na ulinzi wa vyanzo vya maji. 

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa serikali, Taasisi na wananchi kushirikiana katika kuendeleza kilimo chenye tija na rafiki kwa mazingira.


Baadhi ya watumishi wa NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwakatika hafla ya ufungaji wa maonesho ya wakulima (Nanenane 2025) katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma


NEMC YAWAFIKIA WADAU TAKRIBANI 1,450 ELIMU YA MAZINGIRA MAONESHO YA NANENANE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewafikia wadau takriban 1,450  kwa utoaji wa  elimu ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane jijini Dodoma na Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya mwaka huu.

Elimu hiyo imetolewa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Baraza hilo kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika banda lake la maonesho, NEMC ilielimisha kuhusu mbinu bora za kilimo hifadhi kinachozingatia mazingira, ufugaji endelevu, uvuvi salama pamoja na kulinda vyanzo vya maji. 

Aidha, wananchi na wadau waliotembelea hapo walielimishwa kuhusu umuhimu wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ya kilimo  ili kupunguza athari hasi kwa mazingira.

Miongoni mwa masuala yaliyopatiwa kipaumbele ni pamoja na kuwahimiza wawekezaji kusajili miradi NEMC ili kupata vyeti vya mazingira kama kigezo muhimu cha kuendesha shughuli zao kisheria na kwa kuzingatia mazingira.


Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika maonesho ya wakulima, Nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Katika maonesho hayo, wataalamu wa NEMC pia walieleza athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za shughuli za binadamu kama uchomaji moto hovyo, ukataji miti na utupaji taka kwenye mifumo ya ikolojia, hali inayochangia mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa ardhi na upungufu wa rasilimali maji.

“Tunawahimiza wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira. Elimu tunayoitoa ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kiuchumi na kijamii yanayozingatia mustakabali wa mazingira yetu,” alisema Bi. Dalia Kilamlya, Afisa Mazingira NEMC

Kwa ujumla, mwitikio wa wadau mbalimbali katika kupata elimu ya mazingira kutoka NEMC umetajwa kuwa mkubwa na wenye kuleta matumaini ya mabadiliko chanya katika namna jamii inavyoshiriki kwenye kulinda na kuhifadhi mazingira.


Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika Maonesho ya Wakulima, Nanenane 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.


BODI MPYA YA NEMC YAKUTANA NA WATUMISHI– YAHIMIZA UWAJIBIKAJI NA USAFI WA MAZINGIRA

Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imekutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa Taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi  katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.

Mkutano huo umefanyika kwenye kikao cha kawaida cha kila mwezi cha watumishi, ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo, akiambatana na wajumbe wengine sita wa bodi, aliwasihi watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano wa uadilifu, usafi wa mazingira, na utendaji wenye matokeo.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi hao tangu uteuzi wa bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha alisema:

“Ili tuweze kutimiza majukumu yetu ipasavyo kama Taasisi ya mazingira, lazima tuanze na sisi wenyewe kwa kuwa wasafi, wawazi, wenye upendo na tuwe tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za ndani kabla ya kwenda kwa wananchi.”

Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia, majumbani kwa Watoto wadogo na kisha kusambaa kwa jamii nzima. Alisema kuwa bodi itasimamia uwazi katika maamuzi, kushirikiana kwa karibu na menejimenti pamoja na kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wote.

Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Bi. Mwanasha Tumbo (aliyesimama) akizungumza na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Baraza mara baada ya Bodi hiyo kutembelea Ofisi za Baraza  

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alipopata fursa ya kuzungumza aliikaribisha rasmi Bodi hiyo mpya na kueleza kuwa Menejimenti na watumishi wa NEMC wako tayari kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha taasisi inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NEMC inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya wa kimkakati katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.



Matukio katika Picha: Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC na baadhi ya Watumishi wa NEMC wakiwa katika Kikao mara baada ya Bodi kutembelea Ofisi za Baraza Jijini Dar es Salaam.

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekichukulia hatua za kisheria kiwanda bubu cha SUMING kilichopo Mtaa wa Regent Estate katika Kata ya Mikocheni wilayani Kinondoni kinachofanya shughuli za  urejelezaji wa taka hatarishi aina ya simu za   kiganjani chakavu katika eneo la makazi ya watu bila kibali cha kukusanya, kurejeleza, kuhifadhi na kusafirisha taka hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Zoezi hilo limefanyika mara baada ya timu ya wataalamu wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent kukagua kiwanda hicho na kubaini mapungufu yanayokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bi. Glory Kombe amesema ni kosa kisheria kuanzisha kiwanda bila kusajili na kufuata taratibu za kimazingira ikiwepo kuzingatia ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kupata vibali vya kukusanya na kurejeleza taka za kielectroniki. Ameutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kufika mara moja Ofisi za NEMC ili waweze kupata taratibu zinazotakiwa kufuata wakati wa kuanzisha Mradi ili kuepuka madhara ya kimazingira na Afya ya viumbe hai.

Maafisa wa NEMC wakitoa maelezo kwa mmoja wa wamiliki wa Kiwanda hicho

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule ameishukuru NEMC kwa kubaini na kukichukulia hatua Kiwanda hicho na amezitaka Taasisi zote zilizoshiriki ukaguzi wa Kiwanda hicho kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na miongozo ya Taasisi husika.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka Mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji nchini hivyo wawekezaji watumie Mazingira hayo vizuri kwa kufuata utaratibu na Sheria ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama, kuepusha uharibifu wa Mazingira na upotevu wa mapato ya Serikali.

Baraza linaendelea kutoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaoanzisha Viwanda bila kufuata taratibu (Viwanda bubu) ili kuepusha uharibifu wa Mazingira na kulinda Afya ya mazingira na viumbe hai.

Timu ya maafisa wa NEMC, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent wakijadiliana mara baada ya Ukaguzi wa Kiwanda hicho

NEMC YASHIRIKI UKAGUZI WA BWAWA LA TOPESUMU ZAMBIA

Wataalam wa miamba na madini kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Abel Sembeka na Bi. Edika Masisi, wameshiriki katika warsha na ukaguzi wa bwawa la topesumu lililopasuka Februari 15, 2025 kwenye mgodi wa kampuni ya Sino Metal Leach Zambia Limited nchini Zambia.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Jiolojia ya Sweden (SGU) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Lulea kutoka nchini Sweden na Chuo Kikuu cha Copperbelt cha nchini Zambia, huku Wizara ya Madini na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira nchini Zambia (ZEMA) wakiwa wenyeji.

Warsha hiyo umehusisha pia wataalam wa migodi na mazingira kutoka nchi za Afrika Magharibi, Mashariki na Kusini mwa Afrika waliopata mafunzo ya usimamizi wa miamba taka na maji migodini kupitia mradi wa ITP 308 chini ya uratibu wa SGU.

Lengo kuu la warsha hiyo ni kutembelea na kufanya tathmini ya bwawa la topesumu lililopasuka, kujifunza chanzo cha tatizo, mbinu bora za usanifu na usimamizi wa mabwawa ya topesumu, pamoja na hatua za kupunguza madhara kwa mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.






NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...