Nyumbani

WAZIRI MASAUNI AIPONGEZA NEMC UJENZI WA KITUO CHA KUTOA ELIMU YA ZEBAKI - GEITA

 Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yusuf Masauni amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ujenzi wa Jengo la kituo cha kutoa elimu kuhusu athari za afya na mazingira zitokanazo na matumizi yasiyo salama ya Zebaki (Mercury) katika uchenjuaji  wa madini wa dhahabu  kwa wachimbaji wadogo na masuala ya Mazingira kwa ujumla mkoani Geita.

Mhe. Masauni ametoa pongezi hizo Machi 14, 2026 alipozuru eneo la ujenzi wa Jengo hilo ambalo limefikia asilimia 80 ya ujenzi linalojengwa mkabala na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Akizungumza mara baada ya Ukaguzi wa Jengo hilo, Waziri Masauni ameeleza namna alivyofurahishwa na Uzingatiaji wa maswala ya kimazingira katika ujenzi wa Jengo hilo na kwamba litatumika kama Kituo cha kutoa taaluma mbalimbali kwa wananchi kuhusiana na maswala ya Mazingira

"Jengo hili litasaidia masuala mbalimbali ya Mazingira, litakuwa kituo cha kutoa taaluma mbalimbali kwa wananchi kuhusiana na maswala ya Mazingira hususan changamoto kubwa ya matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji wa madini ambapo imekuwa ikiathiri mazingira na afya ya wananchi.

Akizungumza mara baada ya Ukaguzi wa Jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema Jengo hilo ni mfano wa ramani itakayotumika kujenga majengo mengine kumi na mbili (12) ya Kanda za NEMC. Aidha amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Martn Shegella kwa kuipatia NEMC eneo kwa ajili ya ujenzi wa Jengo hilo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP) Dkt. Befrina Igulu ameeleza  Miundombinu rafiki kwa Mazingira iliyowekwa katika Jengo hilo ikiwa ni pamoja na Maabara na Maktaba za kisasa za elimu ya Zebaki mfumo wa nishati ya mwanga asili wa jua, mfumo wa uvunaji wa maji, Ukumbi wa Bodi na Ukumbi mkubwa wa Mikutano.

NEMC imejenga Jengo hilo ikiwa ni manufaa ya Mradi uliolenga kupunguza au kuondosha kabisa matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji wa Madini unafadhiliwa na Global Environment Facility (GEF) na kusimamiwa na Benki ya Dunia ambapo kwa Tanzania unatekelezwa katika Mikoa ya Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe.

NEMC KANDA YA ZIWA VICTORIA MASHARIKI YASHIRIKI ZIARA YA WAZIRI MASAUNI-MWANZA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki ziara ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ya Ukaguzi wa Miradi ya uwekezaji Jijini Mwanza.

Ziara hiyo ililenga kukagua Miradi ya uwekezaji na namna inavyotekeleza Uhifadhi wa Mazingira Mkoani humo.

Akimpokea Mhe. Waziri katika Ofisi yake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Ofisi yake inafanya juhudi kubwa kushirikiana na  NEMC kuhakikisha Mazingira yanalindwa na kutunzwa katika Mkoa huo licha ya changamoto zinazoikabili Ofisi yake hasa katika udhibiti wa Kelele chafuzi za Maeneo ya kumbi za starehe.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya Ukaguzi huo, Mhe. Waziri amewataka wawekezaji na watanzania wote kulinda Mazingira huku akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaosababisha uharibifu wa Mazingira kwa namna yoyote.

"Tunawajibu wa kulinda Mazingira lli Mazingira yawe mazuri ni lazima sisi tuyalinde, na ili yawe mabaya ni lazima sisi tuyaharibu, Serikali inawajibu wa kuhakikisha watanzania wanaendelea kutunza Mazingira" amesema Mhe. Waziri Hamad Yusuf Masauni.



MRADI WA KIHANSI MKOMBOZI WA MAZINGIRA KWA WANANCHI WA MLIMBA

 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuanzia Machi 9 hadi 16 linafanya ufuatiliaji katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Mlimba, Kilolo na Mafinga kwa lengo la kutathmini mafanikio ya Mradi wa Kihansi ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii.

Mradi huo ulitekelezwa kuanzia mwaka 2001 hadi 2019 kupitia awamu tatu ambazo ni Lower Kihansi Environmental Management Project (LKEMP I na II) pamoja na Kihansi Catchment Conservation Management Project (KCCMP). Miradi hiyo ililenga kuimarisha uhifadhi wa baioanuai katika bonde la Kihansi pamoja na kulinda vyanzo vya maji.

Kupitia miradi hiyo, wananchi walipewa elimu ya uhifadhi wa mazingira na kuwezeshwa kufanya shughuli za kilimo nje ya vyanzo vya maji ili kupunguza uharibifu wa mazingira. Miradi hiyo ilitekelezwa chini ya uratibu na usimamizi wa NEMC kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na wadau wengine.

Aidha, wananchi wa Halmashauri hizo waliwezeshwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kupitia vikundi, ikiwemo kilimo cha mpunga, kilimo cha miti, ufugaji wa nyuki na ufugaji wa samaki. Hatua hiyo imechangia kuongeza kipato na kuboresha ustawi wa kaya nyingi katika maeneo hayo.

Kutokana na uwezeshaji huo, baadhi ya wanufaika wamefanikiwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto, kuongeza ukubwa wa mashamba ya kilimo pamoja na kumiliki mifugo, jambo ambalo limeimarisha ustawi wa familia zao na jamii kwa ujumla.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bw. Philiscacius Shaban Masongela, ameishukuru NEMC kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya uhifadhi na uwezeshaji wa kiuchumi. “Kupitia mradi huu nimeweza kuongeza kipato, kujenga nyumba nzuri, kukuza shamba la mpunga na kumiliki mifugo. Hakika mradi huu umeleta mabadiliko chanya katika maisha yetu,” amesema Bw. Masongela.

Naye Bi. Pudensiana Valentine Chagawe kutoka Kikundi cha Nguvu Kazi katika Kijiji cha Chita, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, amesema elimu ya shamba darasa aliyopatiwa kupitia mradi huo imemwezesha kutumia mbinu za kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao. “Awali nilikuwa napata takribani debe 30 (magunia matatu) za mpunga katika nusu heka, lakini baada ya kupata mafunzo ya shamba darasa na kutumia mbinu bora za kilimo, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia debe 180 (magunia 18). Hii imenisaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia yangu,” amesema Bi. Chagawe.

Timu ya NEMC imewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kuendelea kutumia maarifa na ujuzi walioupata kupitia Mradi wa Kihansi katika kuboresha shughuli zao za kiuchumi, kuinua vipato vya familia zao hiki wakitunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗙𝗨𝗡𝗚𝗜𝗔 𝗨𝗝𝗘𝗡𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗘𝗡𝗚𝗢 𝗠𝗔𝗪𝗜𝗟𝗜 𝗠𝗜𝗞𝗢𝗖𝗛𝗘𝗡𝗜

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefungia ujenzi wa majengo mawili yaliyokuwa yanaendelea kujengwa katika eneo la Mikocheni, mtaa wa Regent, mkoani Dar es Salaam, kufuatia ukiukwaji wa taratibu za usimamizi wa mazingira. Majengo yaliyosimamishwa ni pamoja na VIENNATANZANIA CO LTD na TAFBROS LIMITED

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kuwa miradi hiyo ilikuwa inaendelea kuwa na vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA). NEMC imeagiza kusimamishwa mara moja kwa shughuli zote za ujenzi hadi taratibu zote za kisheria zitakapokamilika.

Hata hivyo NEMC imetoa angalizo kwa niradi yote inayoendelezwa bila kufata taratibu za Mazingira kusitisha na kufika ofisi za NEMC kwaajili ya kuanza mchakato wa Uzingatiaji wa Sheria kabla ya kukaguliwa na kupewa adhabu.





NEMC NA THPS WAJADILI USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA AFYA YA JAMII YA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Taasisi ya Tanzania Health Promotion Support (THPS) wamefanya kikao cha pamoja kuhusu ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa mazingira na afya ya jamii tarehe 10 Machi 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza jijini Dar es Salaam. 

Katika kikao hicho, pande zote mbili zimejadiliana na kukubaliana kushirikiana katika kujengea wadau uelewa kuhusu afya ya binadamu na mazingira, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha tafiti kuhusu uhusiano kati ya mazingira na afya ya binadamu, pamoja na kuboresha usimamizi endelevu wa taka zitokanazo na huduma za afya.

Ushirikiano huu unalenga kuunga mkono juhudi za Taifa katika kulinda mazingira, kuboresha afya ya jamii na kuchochea maendeleo endelevu sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza umuhimu wa mazingira salama na jamii yenye afya kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗜 𝗞𝗜𝗞𝗔𝗢 𝗞𝗜𝗟𝗜𝗖𝗛𝗢𝗔𝗡𝗗𝗔𝗟𝗜𝗪𝗔 𝗡𝗔 𝗕𝗘𝗡𝗞𝗜 𝗬𝗔 𝗗𝗨𝗡𝗜𝗔-𝗗𝗢𝗗𝗢𝗠𝗔

𝗟𝗲𝗻𝗴𝗼 𝗻𝗶 𝗸𝘂𝗷𝗮𝗱𝗶𝗹𝗶 𝗨𝘁𝗲𝗸𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮𝗷𝗶 𝘄𝗮 𝗧𝗮𝘁𝗵𝗺𝗶𝗻𝗶 𝘆𝗮 𝗦𝗲𝗸𝘁𝗮 𝘆𝗮 𝗠𝗮𝗱𝗶𝗻𝗶 𝗻𝗰𝗵𝗶𝗻𝗶

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikao kilichoandaliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kilicholenga kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa Tathmini ya Sekta ya Madini nchini inayojulikana kama Mining Sector Diagnostic (MSD) 


Kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Machi 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Best Western jijini Dodoma kiliwakutanisha wadau kutoka Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.

Tathmini ya MSD inalenga kuchambua namna shughuli za Sekta ya madini zinavyotekelezwa na kusimamiwa, hususan kwa kuzingatia masuala ya Sheria, Kanuni, mifumo ya kikodi pamoja na uwezo wa Taasisi mbalimbali za Serikali katika kusimamia Sekta hiyo.

Matokeo ya tathmini ya MSD yataisaidia Benki ya Dunia kutambua kwa kina mchango wa Sekta ya madini katika maendeleo ya Taifa, pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Kupitia matokeo hayo, mapendekezo yatatolewa kuhusu namna bora ya kuimarisha ufanisi wa Sekta hiyo kwa kufanya maboresho ya sera, mifumo ya usimamizi na kuboresha mazingira ya uwekezaji.



NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA NANE WA AFRIMAB NCHINI ZAMBIA

NEMC yashiriki Makutano wa nane wa AfriMab (8th AfriMAB General Assembly) uliofanyika jijini Livingstone, Zambia kuanzia tarehe 9 hadi 13 Machi 2026. Madhumuni ya mkutano huo ni kuendeleza usimamizi endelevu wa hifadhi za bayosfia barani Afrika chini ya kaulimbiu “Kutumia rasilimali za asili za Afrika kupitia teknolojia rafiki kwa mifumo ya ikolojia.” NEMC imewakilishwa na Bi. Marlene Moshi, Afisa Mkuu Mazingira







𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗢𝗡𝗚𝗢𝗭𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗔𝗡𝗢- 𝗪𝗔𝗥𝗦𝗛𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗞𝗔𝗡𝗗𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗜 𝗬𝗔𝗞𝗘 𝗡𝗔 𝗖𝗦𝗘 𝗡𝗔 𝗜𝗡𝗗𝗜𝗔

 𝗡𝗶 𝗞𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗙𝘂𝗿𝘀𝗮 𝘇𝗶𝗹𝗶𝘇𝗼𝗽𝗼 𝗸𝘄𝗲𝗻𝘆𝗲 𝗨𝘀𝗶𝗺𝗮𝗺𝗶𝘇𝗶 𝘄𝗮 𝘁𝗮𝗸𝗮 𝘇𝗮 𝗠𝗮𝘁𝗮𝗶𝗿𝗶 𝗖𝗵𝗮𝗸𝗮𝘃𝘂 Baraza la Ta...