Nyumbani

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗜 𝗞𝗜𝗞𝗔𝗢 𝗞𝗜𝗟𝗜𝗖𝗛𝗢𝗔𝗡𝗗𝗔𝗟𝗜𝗪𝗔 𝗡𝗔 𝗕𝗘𝗡𝗞𝗜 𝗬𝗔 𝗗𝗨𝗡𝗜𝗔-𝗗𝗢𝗗𝗢𝗠𝗔

𝗟𝗲𝗻𝗴𝗼 𝗻𝗶 𝗸𝘂𝗷𝗮𝗱𝗶𝗹𝗶 𝗨𝘁𝗲𝗸𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮𝗷𝗶 𝘄𝗮 𝗧𝗮𝘁𝗵𝗺𝗶𝗻𝗶 𝘆𝗮 𝗦𝗲𝗸𝘁𝗮 𝘆𝗮 𝗠𝗮𝗱𝗶𝗻𝗶 𝗻𝗰𝗵𝗶𝗻𝗶

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikao kilichoandaliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kilicholenga kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa Tathmini ya Sekta ya Madini nchini inayojulikana kama Mining Sector Diagnostic (MSD) 


Kikao hicho kilichofanyika tarehe 10 Machi 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Best Western jijini Dodoma kiliwakutanisha wadau kutoka Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.

Tathmini ya MSD inalenga kuchambua namna shughuli za Sekta ya madini zinavyotekelezwa na kusimamiwa, hususan kwa kuzingatia masuala ya Sheria, Kanuni, mifumo ya kikodi pamoja na uwezo wa Taasisi mbalimbali za Serikali katika kusimamia Sekta hiyo.

Matokeo ya tathmini ya MSD yataisaidia Benki ya Dunia kutambua kwa kina mchango wa Sekta ya madini katika maendeleo ya Taifa, pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Kupitia matokeo hayo, mapendekezo yatatolewa kuhusu namna bora ya kuimarisha ufanisi wa Sekta hiyo kwa kufanya maboresho ya sera, mifumo ya usimamizi na kuboresha mazingira ya uwekezaji.



NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA NANE WA AFRIMAB NCHINI ZAMBIA

NEMC yashiriki Makutano wa nane wa AfriMab (8th AfriMAB General Assembly) uliofanyika jijini Livingstone, Zambia kuanzia tarehe 9 hadi 13 Machi 2026. Madhumuni ya mkutano huo ni kuendeleza usimamizi endelevu wa hifadhi za bayosfia barani Afrika chini ya kaulimbiu “Kutumia rasilimali za asili za Afrika kupitia teknolojia rafiki kwa mifumo ya ikolojia.” NEMC imewakilishwa na Bi. Marlene Moshi, Afisa Mkuu Mazingira







NEMC KANDA YA KASKAZINI YAKAGUA KIWANDA CHA SARUJI CHA MOSHI CEMENT

NEMC Kanda ya Kaskazini yafanya ukaguzi kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Moshi Cement kinachoendeshwa na Kampuni ya JUN YU INVESTMENT INTERNATIONAL CO. LTD kilichopo katika Mkoa wa Kilimanjaro karibu na mpaka wa Horiri. 

Timu ya ukaguzi ilibaini kuwa Kiwanda hicho kina cheti cha TAM, pia kina teknolojia madhubuti ya kudhibiti vumbi na kiwanda chote kimesakafiwa (paved). Hata hivyo kulikuwa na changamoto chache hasa namna ya  udhibiti wa chuma chakavu na usimamizi usiofaa wa madumu yaliyomaliza kemikali. 

Timu ya wataalam ilitoa maelekezo stahiki na muda wa utekelezaji ili kukabiliana na changamoto zilizoibuliwa wakati wa ukaguzi.



𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗜𝗙𝗨𝗡𝗚𝗜𝗔 𝗞𝗜𝗪𝗔𝗡𝗗𝗔 𝗖𝗛𝗔 𝗠𝗔𝗥𝗔 𝗡𝗜𝗟𝗘-𝗣𝗪𝗔𝗡𝗜

Baraza la Taifa la Hifadhi la na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekifunga Kiwanda cha Mara Nile Ltd kilichopo Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani kinachojihusisha na uzalishaji wa kemikali ya Extra Neutral Alcohol (Ethanol) na Carbon dioxide kwa kosa la kutiririsha majitaka yasiyotibiwa  kwenye mazingira

Hatua hiyo imekuja mara baada ya NEMC kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu utiririshaji wa majitaka kwenye Mazingira hali iliyozua taharuki kwa afya za wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bi. Luhuvilo Mwamila amesema awali NEMC ilifanya ukaguzi na kubaini mtambo wa kutibu majitaka usiotumika  badala yake, kiwanda kimekuwa kikitiririsha maji taka yasiyotibiwa moja kwa moja kwenye mazingira na kumwaga tope lenye kemikali hatarishi (sludge).  

Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa kiwanda kimekuwa kikinyonya majitaka na kuyamwaga kwenye machimbo ya mchanga nje ya eneo lao, huku tope sumu wakilichoma katika maeneo hayo hayo.  

Hali hii ni kinyume cha taratibu za mazingira na kuhatarisha afya ya jamii na usalama wa ikolojia. kutotii maelekezo ya mamlaka, hatua kali zimechukuliwa ili kulinda mazingira na afya ya wananchi.



NEMC YAUNGANA NA WANAWAKE DUNIANI KOTE KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE


Wanawake wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutoka Kanda 13 nchini wameungana na wanawake wote duniani kuadhimisha Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, kilichoadhimishwa kitaifa katika Mkoa wa Geita, ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam wanawake wameadhimisha katika Uwanja wa Barafu, Kata ya Mburahati, Wilaya ya Ubungo, ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert John Chalamila.

Maadhimisho hayo yaliyosindikizwa na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwaWanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira ya Maendeleo 2050,” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Albert John Chalamila alisisitiza kuwa maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, kubadilisha mitazamo ya kijamii, na kuchangia moja kwa moja katika malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Aliongeza kuwa kuwepo kwa mazingira rafiki kwa wanawake ni muhimu katika kufanikisha maendeleo jumuishi ya taifa.

Maadhimisho haya yameonyesha wazi kuwa uwezeshaji wa wanawake ni chachu muhimu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, huku akisisitiza kwamba wanawake wanapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ili kuchangia ustawi wa Taifa.






BALOZI LUVANDA AZURU NEMC, AIPONGEZA KWA UWAJIBIKAJI WENYE TIJA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Balozi Baraka Luvanda, amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa uwajibikaji wenye tija katika kutekeleza majukumu yake ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.

Ametoa pongezi hizo leo alipozuru Ofisi za Baraza zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam ikiwa ni ziara yake ya kwanza kwa watumishi wa NEMC tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo. 

Alisema lengo la ziara yake ni kukutana na kuzungumza na watumishi wa Baraza hilo pamoja na kuonesha azma yake chanya ya kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya sekta ya mazingira nchini, hasa ikizingatiwa kuwa mazingira ni eneo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo ni mhimili wa tatu katika maendeleo ya taifa.

“Nimefurahi sana kuona mkitekeleza majukumu yenu kwa ufanisi. Sina shaka maana najua sitakwama mahali popote , mahali hapa pamesheheni wawajibikaji wenye uzalendo wa mazingira nchini mwetu, Tambueni mmepewa jukumu kubwa kwa nchi hii; Mheshimiwa Rais anawaangalia nyinyi zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa watumishi wa NEMC wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu katika kusimamia rasilimali za mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Nyinyi sio wadogo. Mmeonesha kuwa mnaweza kutimiza wajibu wenu kwa uadilifu. Nimefurahi kuona maadili ya kazi yakizingatiwa,” alisisitiza.

Awali, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu na kutambulisha safu ya watumishi wa NEMC, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt Immaculate Sware Semesi alieleza kuwa NEMC kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na Kanuni zake, imekasimiwa  majukumu ya utekelezaji ambayo ndio msingi mzima wa mazingi

Alitaja majukumu hayo kuwa ni kusimamia na kulinda mazingira, kufanya Tathmini ya Athari kwa mazingira (EIA), kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo, kutoa elimu na uhamasishaji wa mazingira, kushauri Serikali kuhusu masuala ya mazingira, kudhibiti uchafuzi wa mazingira, kupokea na kushughulikia malalamiko ya mazingira na kuratibu utekelezaji wa sheria za mazingira

Dkt. Sware alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa watumishi wa NEMC wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kemp ushirikiano wote unaohitajika ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya Taifa

NEMC YASHIRIKI ZIARA YA NAIBU WAZIRI DKT. DUGANGE KAGERA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Festo Dugange kukagua Miradi ya Mazingira katika Halmashauri za Wilaya ya Karagwe na Misenyi Mkoni Kagera.




Ziara hiyo ililenga kuweka bayana Miradi ya kimazingira inayotekelezwa nchini Tanzania ili kufundisha umma wa watanzania namna ambavyo rasilimali za Mazingira zinaweza kuwa fursa za kiuchumi.

Miradi iliyotembelewa inajumuisha Mradi wa Vijana wa kuchakata taka za plastiki, Mradi wa biashara ya kaboni kupitia kilimo mseto (Kinoni Agroforestry Farm) unaotekelezwa na kampuni ya KADERES, Mradi wa Nishati safi ya kupikia na Mradi wa ujenzi wa Dampo la kuhifadhia maji taka Wilayani Karagwe.

Akizungumza na wananchi wakati wa ukaguzi wa Maeneo mbalimbali ya Miradi hiyo, Dkt.  Dugange amehamasisha jamii kuhusu fursa za kiuchumi zinazotokana na Mazingira ikiwemo Biashara ya kaboni pamoja usimamizi sahihi wa taka ngumu kwa ajili ya uchakataji na Urejelezaji. 

"Taka si taka tu bali ni rasilimali muhimu inayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi, taka zinazooza zinaweza kutumika kutengeneza gesi na mbolea ya asili inayoweza kutumika kutengenezea bustani za kioganiki na kupata mazao asilia yasiyo na kemikali na kutunza rutuba ya udongo" Amesema Dkt. Dugange.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi (NEMC) Bw. Boniphace Guni amesema NEMC inaendelea na Usimamizi wa Miradi inayotekelezwa katika Kanda hiyo ikiwemo Mkoa wa Kagera na pia itaendelea kuongeza juhudi za kuhakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inatekelezwa nchini kote ili kuhakikisha Mazingira yanalindwa na kutunzwa.

Aidha, ameisisitiza Jamii kuendelea kutunza Mazingira ili kudhibiti majanga ya kimazingira na kiafya yanayoendelea kushamiri  yakiwemo ongezeko la joto, Upungufu wa Mvua, ukame, na magonjwa.




TIMU YA UKAGUZI WA MAZINGIRA KUTOKA NEMC MAKAO MAKUU NA KANDA YA ZIWA VICTORIA MASHARIKI WAADHIMISHA MEIMOSI 2026 KWA KUPANDA MITI MAKUMBUSHO YA MWL. JULIUS K. NYERERE, BUTIAMA

Timu ya watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wanaofanya ukaguzi wa mazingira katika mikoa ya Kanda ya Zi...