Nyumbani

NEMC YATOA TAHADHARI ZA KIMAZINGIRA KUELEKEA MVUA ZA EL NIÑO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuimarisha utunzaji wa mazingira kuelekea mvua za El Niño, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Akiongea na vyombo vya habari Leo, Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma NEMC Bi. Martha Kawishe amesema mvua ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa, lakini utupaji holela wa taka, kuziba kwa mifereji, ujenzi katika njia za asili za maji na uharibifu wa maeneo oevu vinaweza kuongeza hatari ya mafuriko. Maeneo ya mabondeni, kingo za mito, maeneo yenye miteremko na yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanahitaji tahadhari zaidi.

Ameongeza kuwa Baraza limewataka wananchi kutotupa taka kwenye mifereji, mito na makorongo, huku Mamlaka za Serikali za Mitaa zikihakikisha njia za maji zinasafishwa na kubaki wazi. Aidha, NEMC imesisitiza kulindwa kwa kingo za mito, mabonde na maeneo oevu, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa udongo.

NEMC pia imewataka waendelezaji wa miradi, viwanda, vituo vya mafuta, migodi, hospitali na maeneo yanayohifadhi kemikali au taka hatarishi kuhakikisha vitu hivyo vinasimamiwa kwa usalama ili visisombwe na maji ya mafuriko na kuchafua vyanzo vya maji na makazi ya wananchi.

Baraza limesema litaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine katika kutoa elimu, ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya shughuli zinazoharibu mazingira. NEMC imewahimiza Watanzania kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kuchukua hatua mapema, ikisisitiza kuwa kulinda mazingira ni hatua muhimu katika kupunguza athari za mvua kubwa na mafuriko.

 

𝗗𝗚 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗔𝗧𝗨𝗡𝗨𝗞𝗜𝗪𝗔 𝗧𝗨𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗛𝗘𝗦𝗛𝗜𝗠𝗔–𝗨𝗦𝗜𝗠𝗔𝗠𝗜𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗭𝗜𝗡𝗚𝗜𝗥𝗔

𝗡𝗶 𝗸𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗵𝗶𝘁𝗶𝗺𝗶𝘀𝗵𝗼 𝗹𝗮 𝗞𝗼𝗻𝗴𝗮𝗺𝗮𝗻𝗼 𝗹𝗮 𝗙𝗔𝗥𝗩𝗶𝗕𝗘 𝟮𝟬𝟮𝟲,𝗹𝗶𝗹𝗶𝗹𝗼𝗳𝗮𝗻𝘆𝗶𝗸𝗮 𝗝𝗶𝗷𝗶𝗻𝗶 𝗗𝗮𝗿 𝗲𝘀 𝘀𝗮𝗹𝗮𝗮𝗺

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt.Immaculate Sware Semesi ametunukiwa tuzo ya heshima na Naibu Waziri  Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu - Zanzibar, Mhe. Mboja Ramadhan Mshenga katika Kongamano la kimataifa la Kisayansi la Utafiti wa Uvuvi na Ufugaji wa Samaki kwa Uchumi wa Buluu Endelevu (FARViBE 2026), lililofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 27 Agosti 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa JNICC Jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo iliyopokelewa na Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini Bi. Glory Kombe kwa niaba yake imelenga kutambua mchango alionao katika Sekta ya Mazingira  hasa ikizingatiwa suala la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini ndio msingi wa Maendeleo endelevu kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Naibu Waziri Mhe. Mboja Mshenga amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha juhudi za Uhifadhi na Usimamizi  wa mazingira ya bahari, kwani ndio msingi wa maendeleo katika  sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu huku akisistiza maendeleo ya kiuchumi ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae

NEMC imeshiriki  kongamano hilo kwa lengo la kuwasilisha na kujadili masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira hususani Bahari kwa ustawi wa uvuvi na uchumi wa buluu endelevu.

Kongamano hilo lililowakutanisha wataalamu na wadau wa masuala ya bahari kutoka ndani na nje ya Tanzania, lililenga kujadili tafiti, ubunifu na teknolojia zinazoweza kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.

NEMC NA JNHPP: USIMAMIZI WA MAZINGIRA KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaofanywa  leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la lake la kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira katika miradi ya maendeleo nchini.

Ushiriki wa NEMC katika uzinduzi wa mradi huu wa kimkakati unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa maendeleo ya sekta ya nishati yanaenda sambamba na ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Akieleza ushiriki wa NEMC katika hafla hiyo,  Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema NEMC inaendelea kuhakikisha kuwa utekelezaji wa  mradi wa JNHPP unazingatia Sheria, Kanuni, miongozo na masharti ya mazingira yaliyowekwa.

Amesema katika kutekeleza majukumu yake, NEMC imeendelea kufuatilia uzingatiaji wa masharti ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM), ikiwemo ufuatiliaji wa ubora wa maji, hewa na udongo, usimamizi wa taka, udhibiti wa uchafuzi pamoja na utekelezaji wa hatua za kupunguza athari za kimazingira.

Aidha, NEMC inaendelea kusimamia masuala ya uhifadhi wa bioanuwai, ulinzi wa Mto Rufiji na mifumo yake ya ikolojia, kuhakikisha shughuli za mradi zinafanyika kwa kuzingatia wajibu wa kulinda mazingira na rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

NEMC itaendelea kushirikiana na Serikali, taasisi na wadau mbalimbali katika kuhakikisha JNHPP, kama mradi muhimu wa kimkakati kwa Taifa, unatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu, huku ulinzi wa mazingira ukipewa kipaumbele. NEMC: Mazingira Salama, Maendeleo Endelevu.


#NEMC #JNHPP #Mazingira #MaendeleoEndelevu #Rufiji @nishatisafitz

 

KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAZURU NEMC

📌Yafurahishwa na Mradi wa Kituo cha Gesi Asilia kwa matumizi ya Nishati Safi

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Machano Othman Said, imezuru Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Agosti 20, 2026, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Machano Othman Said, amesema wamefanya ziara NEMC kwa lengo la kuona namna taasisi hiyo inavyoendesha shughuli za kimazingira, kujifunza mafanikio na changamoto zake, pamoja na kubaini maeneo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akikaribisha ugeni huo, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amesema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa mifumo ya ikolojia zinahitaji ushirikiano wa karibu kwa kubadilishana taarifa na uzoefu, kujenga uwezo wa wataalamu na kuandaa programu za pamoja za uhifadhi wa mazingira.

Akifafanua majukumu ya NEMC, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema NEMC inasimamia utekelezaji wa Sheria za mazingira, Tathmini ya Athari kwa Mazingira, udhibiti wa uchafuzi na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa masharti ya mazingira. Amesema Baraza linaendelea kuimarisha ukaguzi, mifumo ya kidijitali, elimu kwa umma na uwezo wa wataalamu katika kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa kwa kuzingatia mazingira.

Katika ziara hiyo, Kamati imetembelea Kituo Mama cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) cha TPDC, Ubungo, na kufurahishwa na mchango wa mradi huo katika matumizi ya nishati safi, kupunguza hewa ukaa na gharama za nishati, hivyo kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.














NEMC, ZEMA ZAPONGEZWA NA MAKAMU WA RAIS KWA KAZI NZURI YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) kwa kazi nzuri ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Mhe. Ndejembi ametoa pongezi hizo kwenye Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) Oktoba 8, 2026 alipotembelea Banda la Maonesho la Taasisi hizo mbili zenye mashirikino katika uhifadhi na usimamizi wa Mazingira nchini.

"Kazi nzuri, hongereni sana" amesema Mhe. Deogratius John Ndejembi.


Ushiriki wa NEMC unaakisi jukumu lake la kisheria na kitaalamu katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa uchafuzi, tathmini ya athari za kimazingira, uzingatiaji wa viwango vya mazingira na ulinzi wa mifumo ikolojia ya bahari na pwani. Kupitia COP12, NEMC inawakilisha masuala ya mazingira ya Tanzania katika majadiliano ya kikanda kuhusu uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuai na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAJI NA MAZINGIRA YAKAGUA HALI YA MAZINGIRA DAMPO LA PUGU NA MTO NG’OMBE DAR ES SALAAM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira leo, Oktoba 17, 2026, imefanya ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Dampo la Pugu Kinyamwezi na Mto Ng’ombe, Dar es Salaam, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, Septemba 18, 2026, kuhusu hatua za kukabiliana na changamoto za kimazingira katika maeneo hayo.


Akizungumza baada ya ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Prof. Pius Zebhe Yanda (Mb) ameelekeza kuwepo kwa mpango madhubuti wa kudhibiti na kusimamia Dampo la Pugu na kusisitiza umuhimu wa kutathmini afya za wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo ikiwa ni  pamoja na kuweka uzio ili kuhakikisha makazi ya Wananchi hayasogei karibu na dampo hilo 

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ameeleza kuwa Serikali haina budi kuweka mwekezaji atakayeshughulikia uchakataji wa taka katika Dampo la Pugu, hatua inayotarajiwa kuboresha usimamizi wa taka na kupunguza athari za kimazingira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Aidha, ameielekeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana kwa karibu na taasisi zote zinazohusika, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuhakikisha mradi wa dampo hilo haukwami.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mhe. Albert Chalamila, akiwasilisha taarifa fupi kuhusu hali ya Mazingira amesema Mkoa wa Dar es Salaam una takribani kilomita za mraba 1300 na watu zaidi ya Milioni  tano na laki tatu kwa mujibu wa sensa ya Mwaka 2022 hali inayopelekea uzalishaji mkubwa wa taka kwa siku na kutokana miundombinu kupelekea kiwango kidogo cha taka kupelekea dampo.



𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa kufanyika Septemba 15–16, 2026 Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujadili mikakati ya kuhakikisha unaleta tija katika ajenda ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema ushirikiano kati ya NEMC na TGS ni muhimu katika kuongeza uelewa, ubunifu na ushiriki wa wadau, hususan vijana, katika kutafuta suluhisho la changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

"NEMC, kama mlezi wa Tanzania Green Summit, ataendelea kuunga mkono majukwaa yanayochochea uendelevu wa mazingira, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na ushiriki wa vijana katika ajenda ya mazingira na maendeleo endelevu" amesisitiza Dkt.Sware Semesi

Tanzania Green Summit 2026 yenye kaulimbiu “𝙆𝙪𝙜𝙚𝙪𝙯𝙖 𝙃𝙖𝙩𝙪𝙖 𝙯𝙖 𝙏𝙖𝙗𝙞𝙖𝙣𝙘𝙝𝙞 𝙆𝙪𝙬𝙖 𝙁𝙪𝙧𝙨𝙖” inatarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 1,000 kutoka sekta mbalimbali kujadili na kuibua fursa za ubunifu, uwekezaji, ajira, ushirikiano na maendeleo endelevu zinazotokana na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ushirikiano kati ya NEMC na TGS unaendana na Mpango Mkakati wa NEMC pamoja na malengo ya Dira ya Tanzania ya 2050, hususan katika kujenga uchumi endelevu, thabiti, wa kibunifu na jumuishi unaozingatia fursa zinazotokana na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.







NEMC YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kujadili utekelezaji wa baj...