Nyumbani

NEMC KANDA YA ILALA YAKUTANA NA UONGOZI WA BENKI YA EQUITY KUJADILI FURSA ZA MAZINGIRA

 

NEMC Kanda ya Ilala, imekutana na uongozi wa Benki ya Equity kwa lengo la kujadili fursa za mashirikiano zilizopo katika sekta ya mazingira pamoja na utoaji wa elimu ya fedha. 

Kikao hicho kilichofanyika Januari 04, 2026 katika ofisi za NEMC jijini Dar es Salaam, kimeongozwa na Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Ilala, Bi. Abela Muyungi, na kuwahusisha Meneja wa Tawi la Equity–Nyerere Road pamoja na Meneja wa Mahusiano wa benki hiyo. Majadiliano hayo yamejikita katika utoaji wa elimu ya mazingira, matumizi ya nishati safi, uzingatiaji wa sheria na kanuni za mazingira katika viwanda, pamoja na huduma za kifedha.




DKT. SEMESI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUDHIBITI MATUMIZI YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU (EHPMP)

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Sware Semesi ameonesha kuridhishwa na mambo mazuri yanayofanywa kupitia Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP).

Dkt. Semesi ameonesha kuridhishwa huko Februari 2,2026 jijini Dodoma alipokuwa akitoa neno wakati akifungua kikao cha kupitia taarifa za Utekelezaji wa Mradi huo kilichohusisha timu ya wataalamu wa Utekelezaji wa Mradi, timu ya wataalamu kutoka Bank ya Dunia na Wajumbe wengine kutoka Taasisi mbalimbali na Wizara.

Dkt. Semesi amesema Mradi huo sio tu una manufaa katika kupunguza matumizi ya Zebaki lakini pia una faida nyingi zaidi.


"Matokeo tayari yanaonekana na yanasababisha mabadiliko katika sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia mbadala wa zebaki. EHPMP haihusu tu kupunguza matumizi ya zebaki; inahusu kubadilisha sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu. Inalenga kulinda wachimbaji madini na familia zao, kukuza urasimishaji na utawala bora, kuimarisha utunzaji wa mazingira, na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi. Hatimaye, inalenga kuhakikisha kwamba utajiri unaotokana na dhahabu ya Tanzania unaenda sambamba na matumizi salama ambayo yanalinda afya ya umma na mazingira." Amesema Dkt. Semesi.

Akizungumzia kuhusu Utekelezaji wa Mradi huo, Dkt. Semesi hakusita kusema kuhusu uratibu mzuri unaofanywa kwa kushirikiana baina ya NEMC na Benki ya Dunia hali iliyopelekea matokeo hayo chanya ya Utekelezaji wa Mradi huo.


"Kufikia leo, utekelezaji umefikia 84% ya vipengele vilivyopangwa, kuonyesha maendeleo makubwa kuelekea malengo ya mradi. Hii inajengwa juu ya msingi uliowekwa na Benki ya Dunia na NEMC kwa kuwa na usimamizi thabiti na kuhakikisha kwamba afua za mradi zinafikiwa kwa ufanisi zaidi." Ameongezea Dkt. Semesi.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesimamia mradi huu wa miaka minne tangu Oktoba 2020 na umekuwa ukitekelezwa katika mikoa 7 ambayo ni Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe. Awali Mradi uliopangwa kufungwa Julai 2025, mradi umeongezwa hadi mwezi Machi, 2026 ili kuruhusu kukamilika kwa vipengele muhimu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Uhamasishaji cha Zebaki na Kituo Mbadala cha Zebaki. Nyenzo hizi ni muhimu ili kuhakikisha kupitishwa kwa teknolojia salama, kukuza mbinu zisizo na zebaki, na kuanzishwa kwa Kituo cha Ubora.







NEMC NA TAASISI ZA KISERIKALI NA ZISIZO ZA KISERIKALI WAFANYA MAPITIO YA MPANGO KAZI WA BARAZA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na wadau kutoka taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali wameshirikiana kutoa maoni kwenye Mpango mkakati mpya (Strategic Plan) wa Mwaka 2026/2027-2030/2031 ikiwa ni hatua mojawapo  ya kuhakikisha utendaji kazi wa Baraza wenye tija na manufaa kwa muktadha wa utunzaji wa Mazingira.

Akifungua Kikao hicho, Februari 3, 2026, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw. Dickson Mjinja kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculate Sware Semesi aliwashukuru washiriki wote kwa kujitoa na kufika kwa wingi ili kufanikisha dhumuni la Kikao hicho muhimu chenye tija katika Utekelezaji wa majukumu ya Baraza.











NEMC KANDA YA KUSINI YASHIRIKI WARSHA YA UWAJIBIKAJI SEKTA YA UZIDUAJI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini limeshiriki katika Warsha ya kuelimisha umma kuhusu uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya Uziduaji, iliyofanyika Februari 2, 2026 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.


Katika warsha hiyo, Bw. Obasanjo Nniwako (SEO) aliwasilisha mada kuhusu utunzaji wa mazingira na Uzingatiaji wa Sheria na kanuni za mazingira katika shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia. Huku mgeni rasmi akikuwa ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Ndugu Terence Ngole, aliyemwakilisha Waziri wa Madini, Mheshimiwa Antony Mavunde.

NEMC iliwahimiza wachimbaji wa kati na wadogo, hususan kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake ili kuepusha athari za mazingira, huku ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka taratibu hizo





NEMC YAFANYA UFUATILIAJI WA MRADI WA KCCMP

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya ufuatiliaji wa baada ya utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi na Usimamizi wa Bonde la Kihansi (KCCMP) kuanzia tarehe 19 hadi 30 Januari 2026 katika wilaya za Mlimba, Kilolo na Mufindi.

Mradi huo ulitekelezwa kati ya 2013 hadi 2019, ukiwa na lengo la kuimarisha uhifadhi wa bioanuai na kulinda viumbe hai adimu kama Chura wa Kihansi (Kihansi Spray Toad), sambamba na kusimamia rasilimali za maji kwa uendelevu.

Timu ya NEMC iliongozwa na Bw. Paul Kalokola, ikishirikiana na maafisa wa halmashauri na taasisi kama UDSM, SUA, TAWIRI, TANESCO na Ofisi ya Bonde la Rufiji. Walitembelea vituo vya uzalishaji na urejeshwaji wa Chura wa Kihansi na maeneo ya mradi kujionea utekelezaji.

Ripoti ya NEMC itatoa mapendekezo ya kitaalamu kuhakikisha uendelevu wa matokeo ya mradi na uhifadhi wa Bonde la Kihansi kwa muda mrefu.













WAALAMU WA KUDHIBITI MATUMIZI YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO (NEMC) NA WATAALAMU KUTOKA BENKI YA DUNIA WAKUTANA NA DKT. MUYUNGI

 

Timu ya wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inayosimamia Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP) wakiongozwa na Mratibu wa mradi huo Mhandishi Dkt. Befrina Igulu wakiwa na timu ya wataalamu kutoka Benki ya Dunia wamekutana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi Februari 2,2026 kwenye Ofisi zilizopo katika jengo la NHIF jijini Dodoma.

Wataalamu hao NEMC na Benki ya Dunia wamekutana na Dkt. Muyungi kwa lengo la kutathmini uendelevu wa mradi na kuhakikisha uzingatiaji wa mikataba ya kimataifa.

Aidha, majadiliano yaligusia upatikanaji wa rasilimali fedha za ziada kwa ajili ya usimamizi wa taka za kielektroniki ambazo zina uhusiano wa karibu na athari za madini joto kama zebaki.

Benki ya Dunia na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi kwa pamoja wamepongeza hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya msingi ya utekelezaji wa mradi huu.

#ehpmp #environmentalhealth #worldbank #mercuryfree







NEMC, HALMASHAURI YA JIJI LA DAR ES SALAAM NA WADAU WA MAZINGIRA WASAFISHA FUKWE YA DENGU

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ilala  limeshirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na wadau mbalimbali wa Mazingira kusafisha fukwe ya Dengu iliyopo Kata ya Kivukoni, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo lililofanyika leo Januari 31, 2026 lililenga kuimarisha usafi wa mazingira na kulinda fukwe dhidi ya uchafuzi pamoja na kuboresha mandhari ya jiji, hususan Wilaya ya Ilala ambayo ni lango kuu la kupokea wageni wanaoingia nchini kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Bandari ya Dar es Salaam pamoja na Stesheni ya Treni.

Mgeni rasmi katika zoezi hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuendeleza usafi wa mazingira kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Wilaya ya Ilala inaendelea kuwa safi, salama na yenye kuvutia.

Amesema ushiriki wa wadau katika shughuli za usafi wa mazingira ni nguzo muhimu ya kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira ya fukwe na kuchangia maendeleo endelevu ya jiji na taifa kwa ujumla.




BODI YA WAKURUGENZI NEMC YAFANYA MAPITIO YA MPANGO MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA MIAKA MITANO

Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC pamoja na Menejimenti wamefanya kikao katika Ukumbi wa Hoteli ya Adden Palace jijini Mwanza kufanya mapitio ya p...