Nyumbani

NEMC YAWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAKE KUELEKEA COP31

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wake kuhusu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), michakato ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba huo (COP), pamoja na nafasi ya NEMC katika kuendeleza vipaumbele vya kitaifa vya Tanzania kuhusu mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama (COP31).

Mafunzo hayo yalijikita katika michakato muhimu ya UNFCCC, vipaumbele vya Tanzania kuelekea COP31, nafasi na majukumu ya NEMC katika mikutano ya COP, pamoja na fursa za ushiriki wa kimkakati katika majadiliano na maamuzi ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo, Bw. Fredrick Mulinda kutoka NEMC na Dkt. Sixbert Mwanga kutoka Shirika la Climate Action Network (CAN) Tanzania, waliwajengea uwezo watumishi kuhusu maeneo muhimu ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, vipaumbele vya kitaifa katika majadiliano pamoja na fursa zinazoweza kuwepo kwa maslahi yaTanzania. Aidha, wawezeshaji waliangazia mikakati ya kutumia fursa za upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga mashirikiano na kuimarisha ushiriki wa kitaasisi katika kutekeleza vipaumbele vya taifa.

NEMC, ikiwa ni taasisi ya kitaifa yenye jukumu la kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira, na taasisi yenye ithibati ya kupata na kusimamia fedha kutoka Mifuko ya Kimataifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund (AF) na Green Climate Fund – GCF), ina nafasi muhimu katika kuhamasisha na kuratibu upatikanaji wa fedha za tabianchi, kuimarisha usimaizi wa mazingira na kusaidia jamii za Kitanzania kuongeza uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Usimamizi wa Mazingira, Dkt. Caren Kahangwa, aliwashukuru washiriki kwa ushiriki wao mzuri na kuwasisitiza kuendelea kujenga uelewa, kufuatilia maendeleo ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kujiandaa kikamilifu kwa ushiriki wenye tija katika mikutano ya COP unaokaribia kuanza.


NEMC YASISITIZA UWEKEZAJI ENDELEVU UNAOZINGATIA UHIFADHI WA MAZINGIRA; MKUTANO WA USHIRIKIANO WA URUSI NA AFRIKA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika Mkutano wa “Russia–Africa Summit” pamoja na Jukwaa la Business to Business (B2B) ulioanza Oktoba 22 hadi 29, 2026 na kufunguliwa rasmi na Rais wa Urusi, Vladmir Putin katika jiji la Moscow nchini Urusi. Mkutano huo umezikutanisha nchi 48 za Afrika na wawekezaji kutoka Urusi kwa mazungumzo ya kibiashara na uwekezaji, ikiwemo kuingia ubia na Tanzania.

NEMC ilieleza nafasi yake kama taasisi inayosimamia uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, huku ikitangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya mazingira na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji unaozingatia ulinzi wa mazingira, pamoja na kujenga mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi. NEMC, kwa kushirikiana na TIB Development Bank na Jitegemee Holdings, ilishiriki kikao cha pamoja na Uralsib Bank nchini Urusi na kujadili juu ya miradi inayolenga kubadilisha taka kuwa nishati na nishati jadidifu.

Katika Mkutano huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, aliwakilisha ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ujumbe huo ulihusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia na Urusi, hasa katika teknolojia ya kidijitali, nishati na madini, pamoja na kuvutia uwekezaji wa Urusi katika mbolea, madawa na elimu ya ufundi. Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, hivyo uchumi wa kidijitali ni kipaumbele cha taifa, na Tanzania inatarajia kuendeleza ushirikiano na Urusi katika nyanja hizo.

Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika kongamano hilo umeleta manufaa kwa taasisi, ikiwemo kupanua mtandao wa kitaasisi na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya mazingira, kuimarisha uwezo wake wa kusimamia masuala ya mazingira nchini, na kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa sera za mazingira. Aidha, ushiriki huo umeimarisha nafasi ya NEMC kama taasisi muhimu katika kuvutia uwekezaji endelevu na kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania yanaenda sambamba na ulinzi wa mazingira kwa manufaa ya sasa na baadae.








NEMC YASHIRIKI SEMINA YA VIWANDA TNCC MKOA WA PWANI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Oktoba 28, 2026 limeshiriki semina ya viwanda iliyoandaliwa na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) mkoani Pwani, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za viwanda na wajibu wa wafanyabiashara katika utunzaji wa mazingira.

Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesisitiza umuhimu wa kuwasikiliza wafanyabiashara na kuwaelimisha kuhusu wajibu wao ili waweze kuelewa majukumu yao na kushirikiana na Serikali kufikia malengo ya pamoja. Aidha, ameeleza kuwa changamoto zilizowasilishwa, ikiwemo hali mbovu ya miundombinu ya barabara zinazoelekea viwandani, zitazingatiwa na kufanyiwa kazi.

Kwa upande wake, Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini NEMC, Bi. Glory Kombe, ameeleza kuwa NEMC inaendelea kutoa elimu na ushauri kwa wamiliki na waendeshaji wa viwanda kuhusu taratibu za usajili, umuhimu wa kupata Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira pale kinapohitajika, pamoja na kuzingatia masharti ya cheti hicho. Elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wadau kuelewa matakwa ya kisheria na namna bora ya kuendesha shughuli zao bila kuathiri mazingira.

Kuhusu ukaguzi wa mazingira, NEMC hufanya ukaguzi katika maeneo ya viwanda ili kuthibitisha utekelezaji wa masharti yaliyowekwa katika vibali na vyeti vya mazingira, pamoja na kubaini changamoto zinazoweza kusababisha uchafuzi wa mazingira. Kupitia elimu na ukaguzi, NEMC inalenga kuimarisha uzingatiaji wa sheria za mazingira, kuzuia uchafuzi, kulinda afya za wananchi na kuhakikisha shughuli za viwanda zinaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu.



TANZANIA, GEF KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA UHIFADHI WA BIOANUWAI

Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha, kujenga uwezo wa kitaasisi na kuendeleza miradi ya uhifadhi wa bioanuwai na mazingira nchini.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha miradi inayopendekezwa inaandaliwa kwa ubora unaostahili, inakidhi vigezo vya ufadhili na inatekelezwa kwa ufanisi na uendelevu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa GEF, Diego Mesa Puyo, pembezoni mwa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai, uliofanyika jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 28, 2026.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania imependekeza kuanzishwa kwa majadiliano ya kitaalamu kati ya GEF, Ofisi ya Makamu wa Rais na taasisi husika za kisekta, ikiwemo taasisi zinazotekeleza miradi, ili kubaini mahitaji ya kifedha na kuweka vipaumbele vya uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira.

Aidha, Tanzania imeiomba GEF kutoa mwongozo kuhusu namna ya kuoanisha miradi inayopendekezwa na mwelekeo wa programu za mfuko huo, vigezo vya kustahili ufadhili pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika hatua za maandalizi na utekelezaji wa miradi.

Katika kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha, Tanzania pia imependekeza kuwepo kwa mikakati ya pamoja ya kuhamasisha fedha kutoka Serikalini, kwa washirika wa maendeleo, mashirika ya uhifadhi na sekta binafsi inayowajibika.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa vyanzo vya fedha na kuongeza uwezo wa kugharamia miradi ya uhifadhi wa bioanuwai na mazingira kwa muda mrefu.

Vilevile, Tanzania imehimiza majadiliano kuhusu mifumo endelevu ya ufadhili wa uhifadhi, ikiwemo uanzishwaji wa mifuko ya dhamana ya uhifadhi, malipo kwa huduma za mifumo ikolojia na uwekezaji unaochangia uhifadhi wa mazingira, huku ukizingatia ulinzi wa mazingira na maslahi ya jamii.

Katika hatua nyingine, Tanzania imeiomba GEF kuongeza msaada wa kitaalamu na kitaasisi kwa Ofisi ya Uratibu ya Kituo cha Kitaifa cha Uendeshaji wa GEF






WAZIRI MASAUNI AWATAKA WADAU KUTUMIA SOKO LA KABONI KUANZISHA MIRADI YENYE TIJA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amewataka wadau wa maendeleo nchini kutumia Soko la Kaboni kuanzisha miradi inayoweza kufadhilika, mifumo inayotabirika na uwekezaji unaopimika.

Waziri Masauni ameyasema hayo Oktoba 22, 2026 Hyatt Regency akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania lililokuwa na kaulimbiu isemayo "Siku Moja, Soko Moja, Maono ya Pamoja" lililokusanya wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili mambo mbalimbali yahusuyo biashara ya Kaboni.

"Jukwaa hili lisiishie kuwa mahali pa kubadilishana mawazo, liwe mwanzo wa ushirikiano unaozaa miradi inayofadhilika, mifumo inayotabirika na uwekezaji unaopimika." Amesema Waziri Masauni.

Aidha, Waziri Masauni ameongeza kwa kusema kuwa kila mdau aliyefika kwenye Jukwaa hilo atoke na hatua mahsusi: mwekezaji  akiwa na mradi wa kuwasilisha, taasisi ya umma ikiwa na fursa ya kutathmini, taasisi ya fedha ikiwa na bidhaa ya kufadhili, na NCMC ikiwa na orodha ya ahadi za kufuatilia.

"Nitaomba NCMC iniletee taarifa ya matokeo ya Jukwaa hili ndani ya siku thelathini. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa mapato na manufaa yatokanayo na miradi yanaendana na Sheria, mikataba na masharti ya uidhinishaji, huku maslahi ya Taifa na ya jamii yakilindwa." Amesisitiza Waziri Masauni.

NEMC imeshiriki Jukwaa hilo ikiwa ni Taasisi inayosimamia masuala ya Mazingira nchini ambapo Watumishi kadhaa wameshiriki wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira, Dkt. Careen Kahangwa.











MKURUGENZI MKUU WA NEMC ASHIRIKI COP17 KUIMARISHA UHIFADHI WA BIOANUWAI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi, anashiriki Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (CBD COP17), unaofanyika Yerevan, Armenia.

Ushiriki wa NEMC katika mkutano huu unalenga kuimarisha usimamizi wa mazingira, uhifadhi wa bioanuwai na uhamasishaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa programu za uhifadhi na urejeshaji wa mifumo ya ikolojia nchini Tanzania.

Kupitia mkutano huu, NEMC inatafuta kuimarisha ushirikiano na wadau wa kimataifa, taasisi za ufadhili na washirika wa maendeleo ili kuendeleza mbinu endelevu za kugharamia uhifadhi, kuboresha ufuatiliaji wa hali ya mazingira na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za asili.

NEMC pia inasisitiza umuhimu wa kuunganisha uhifadhi wa bioanuwai na maendeleo ya kiuchumi, ajira za kijani, usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na pwani, pamoja na ushiriki wa jamii katika kulinda mazingira.

Aidha, NEMC inaona fursa ya kuendeleza miradi inayounganisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo ya misitu, mikoko, ardhioevu, vyanzo vya maji na mifumo mingine muhimu ya ikolojia.

Dkt. Semesi anasisitiza kuwa: “Uhifadhi wa bioanuwai unahitaji ushirikiano wa wadau wote, uwekezaji wa kutosha na mifumo imara ya usimamizi na ufuatiliaji wa mazingira. Ni muhimu kuhakikisha kuwa rasilimali za kifedha zinazopatikana zinasaidia utekelezaji wa hatua halisi za uhifadhi, urejeshaji wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.”

NEMC itaendelea kutumia fursa zinazotokana na COP17 kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhamasisha rasilimali zitakazosaidia Tanzania kutekeleza vipaumbele vyake vya uhifadhi wa bioanuwai na usimamizi endelevu wa mazingira.

Mkurugenzi Mkuu NEMC ameambatana na Mhe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni (Mb)

NEMC YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kujadili utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2026/27 katika sekta ya Madini.

Katika wasilisho hilo, masuala ya udhibiti wa athari za kimazingira zitokanazo na shughuli za uchimbaji madini, usimamizi wa taka migodini, urejeshaji wa maeneo yaliyoathiriwa na uchimbaji pamoja na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za mazingira ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele katika mipango na utekelezaji wa bajeti.

Kamati imeelekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya NEMC na wadau wa sekta ya Madini  katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na misingi ya maendeleo endelevu.

Majadiliano hayo yanalenga kuimarisha usimamizi wa mazingira ili rasilimali za madini ziendelee kuchangia maendeleo ya taifa huku mazingira yakilindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.








𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐍𝐆'𝐀𝐑𝐀 𝐊𝐖𝐄𝐍𝐘𝐄 𝐑𝐈𝐀𝐃𝐇𝐀 - 𝐒𝐇𝐈𝐌𝐌𝐔𝐓𝐀 𝟐𝟎𝟐𝟔

📌𝐘𝐚𝐭𝐢𝐧𝐠𝐚 𝐍𝐮𝐬𝐮 𝐟𝐚𝐢𝐧𝐚𝐥𝐢 𝐌𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐌𝐢𝐭𝐚 𝟏𝟎𝟎, 𝐌𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐯𝐢𝐣𝐢𝐭𝐢, 𝐦𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐦𝐚𝐠𝐮𝐧𝐢𝐚 𝐧𝐚 𝐟𝐚𝐢...