Nyumbani

NEMC YAUNGA MKONO MAAGIZO YA MKUU WA MKOA KUHUSU TAKA SIFURI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, kuhusu utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Kata za Chamazi na Toangoma, Meneja wa Kanda ya Temeke wa NEMC, Bw. Abel Sembeka, alisema NEMC inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutenganisha taka katika chanzo na kuhakikisha taka zinazoweza kurejelezwa, kama plastiki, karatasi, vyuma na vioo, zinakusanywa na kupelekwa kwa wachakataji badala ya kutupwa ovyo.

Ameongeza kuwa maagizo hayo yanaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama na endelevu, huku jamii ikihamasishwa kupunguza uzalishaji wa taka, kutenganisha taka katika vyanzo na kuimarisha urejelezaji wa taka ili ziweze kutumika tena kama malighafi na fursa ya kiuchumi ndani ya mzunguko wa uchumi wa kijani

NEMC imeahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Temeke na wadau wengine wa Mazingira katika kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri, hususan katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu urejelezaji na matumizi ya taka kama rasilimali, kwa lengo la kupunguza taka zinazopelekwa dampo na kujenga Dar es Salaam safi na yenye mazingira endelevu.












Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa ...