Nyumbani

NEMC YASHIRIKI HAFLA YA UFUNGAJI WA MAONESHO YA NANENANE, RAIS AONGEZA SIKU MBILI ZA KUTOA HUDUMA UWANJANI HAPO

Baraza la Taifa la Hifadhi na  Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu kwenye hafla ya ufungaji wa maonesho ya 32 ya wakulima (Nanenane) Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma leo

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo katika hotuba yake  amesisitiza umuhimu wa kilimo bora na endelevu kama mhimili wa maendeleo ya Taifa. 

Amesema sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi  ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, hivyo zinahitaji uwekezaji wa kutosha, ubunifu na usimamizi madhubuti ili kuijenga kesho bora kwa Watanzania wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiwasili katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma kufunga Maonesho ya Wakulima (Nanenane 2025) katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Ameelekeza Wizara ya Kilimo kuimarisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima, pamoja na kuunganisha nguvu katika kukuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan  ametangaza kuongeza siku mbili zaidi za maonesho hadi tarehe 10 Agosti ili kutoa nafasi kwa wananchi na wadau kuendelea kupata huduma na elimu mbalimbali.

" Maonesho haya ni siku nane, lakini kiuhalisia siku nane hazitimii kwani maandalizi yanachelewa, hivyo kuanzia mwaka ujao maandalizi ya maonesho yaanze tarehe 25/07." Ameelekeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan

Hafla hiyo ya ufungaji imehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu, Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Binafsi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa Maonesho ya Wakulima (Nanenane 2025) katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Kwa upande wake, NEMC ilitumia maonesho haya kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira katika shughuli za kilimo na ufugaji, ikiwa ni pamoja na matumizi salama ya  mbolea, upandaji miti, na ulinzi wa vyanzo vya maji. 

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa serikali, Taasisi na wananchi kushirikiana katika kuendeleza kilimo chenye tija na rafiki kwa mazingira.


Baadhi ya watumishi wa NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwakatika hafla ya ufungaji wa maonesho ya wakulima (Nanenane 2025) katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma


NEMC YAWAFIKIA WADAU TAKRIBANI 1,450 ELIMU YA MAZINGIRA MAONESHO YA NANENANE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewafikia wadau takriban 1,450  kwa utoaji wa  elimu ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane jijini Dodoma na Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya mwaka huu.

Elimu hiyo imetolewa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi za Baraza hilo kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika banda lake la maonesho, NEMC ilielimisha kuhusu mbinu bora za kilimo hifadhi kinachozingatia mazingira, ufugaji endelevu, uvuvi salama pamoja na kulinda vyanzo vya maji. 

Aidha, wananchi na wadau waliotembelea hapo walielimishwa kuhusu umuhimu wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ya kilimo  ili kupunguza athari hasi kwa mazingira.

Miongoni mwa masuala yaliyopatiwa kipaumbele ni pamoja na kuwahimiza wawekezaji kusajili miradi NEMC ili kupata vyeti vya mazingira kama kigezo muhimu cha kuendesha shughuli zao kisheria na kwa kuzingatia mazingira.


Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika maonesho ya wakulima, Nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Katika maonesho hayo, wataalamu wa NEMC pia walieleza athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za shughuli za binadamu kama uchomaji moto hovyo, ukataji miti na utupaji taka kwenye mifumo ya ikolojia, hali inayochangia mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa ardhi na upungufu wa rasilimali maji.

“Tunawahimiza wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira. Elimu tunayoitoa ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kiuchumi na kijamii yanayozingatia mustakabali wa mazingira yetu,” alisema Bi. Dalia Kilamlya, Afisa Mazingira NEMC

Kwa ujumla, mwitikio wa wadau mbalimbali katika kupata elimu ya mazingira kutoka NEMC umetajwa kuwa mkubwa na wenye kuleta matumaini ya mabadiliko chanya katika namna jamii inavyoshiriki kwenye kulinda na kuhifadhi mazingira.


Elimu ya Mazingira ikitolewa kwa wageni waliotembelea banda la NEMC katika Maonesho ya Wakulima, Nanenane 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.


BODI MPYA YA NEMC YAKUTANA NA WATUMISHI– YAHIMIZA UWAJIBIKAJI NA USAFI WA MAZINGIRA

Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imekutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa Taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi  katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.

Mkutano huo umefanyika kwenye kikao cha kawaida cha kila mwezi cha watumishi, ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo, akiambatana na wajumbe wengine sita wa bodi, aliwasihi watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano wa uadilifu, usafi wa mazingira, na utendaji wenye matokeo.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi hao tangu uteuzi wa bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha alisema:

“Ili tuweze kutimiza majukumu yetu ipasavyo kama Taasisi ya mazingira, lazima tuanze na sisi wenyewe kwa kuwa wasafi, wawazi, wenye upendo na tuwe tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za ndani kabla ya kwenda kwa wananchi.”

Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia, majumbani kwa Watoto wadogo na kisha kusambaa kwa jamii nzima. Alisema kuwa bodi itasimamia uwazi katika maamuzi, kushirikiana kwa karibu na menejimenti pamoja na kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wote.

Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Bi. Mwanasha Tumbo (aliyesimama) akizungumza na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Baraza mara baada ya Bodi hiyo kutembelea Ofisi za Baraza  

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alipopata fursa ya kuzungumza aliikaribisha rasmi Bodi hiyo mpya na kueleza kuwa Menejimenti na watumishi wa NEMC wako tayari kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha taasisi inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NEMC inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya wa kimkakati katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.



Matukio katika Picha: Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC na baadhi ya Watumishi wa NEMC wakiwa katika Kikao mara baada ya Bodi kutembelea Ofisi za Baraza Jijini Dar es Salaam.

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekichukulia hatua za kisheria kiwanda bubu cha SUMING kilichopo Mtaa wa Regent Estate katika Kata ya Mikocheni wilayani Kinondoni kinachofanya shughuli za  urejelezaji wa taka hatarishi aina ya simu za   kiganjani chakavu katika eneo la makazi ya watu bila kibali cha kukusanya, kurejeleza, kuhifadhi na kusafirisha taka hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Zoezi hilo limefanyika mara baada ya timu ya wataalamu wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent kukagua kiwanda hicho na kubaini mapungufu yanayokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bi. Glory Kombe amesema ni kosa kisheria kuanzisha kiwanda bila kusajili na kufuata taratibu za kimazingira ikiwepo kuzingatia ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kupata vibali vya kukusanya na kurejeleza taka za kielectroniki. Ameutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kufika mara moja Ofisi za NEMC ili waweze kupata taratibu zinazotakiwa kufuata wakati wa kuanzisha Mradi ili kuepuka madhara ya kimazingira na Afya ya viumbe hai.

Maafisa wa NEMC wakitoa maelezo kwa mmoja wa wamiliki wa Kiwanda hicho

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule ameishukuru NEMC kwa kubaini na kukichukulia hatua Kiwanda hicho na amezitaka Taasisi zote zilizoshiriki ukaguzi wa Kiwanda hicho kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na miongozo ya Taasisi husika.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka Mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji nchini hivyo wawekezaji watumie Mazingira hayo vizuri kwa kufuata utaratibu na Sheria ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama, kuepusha uharibifu wa Mazingira na upotevu wa mapato ya Serikali.

Baraza linaendelea kutoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaoanzisha Viwanda bila kufuata taratibu (Viwanda bubu) ili kuepusha uharibifu wa Mazingira na kulinda Afya ya mazingira na viumbe hai.

Timu ya maafisa wa NEMC, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent wakijadiliana mara baada ya Ukaguzi wa Kiwanda hicho

NEMC YASHIRIKI UKAGUZI WA BWAWA LA TOPESUMU ZAMBIA

Wataalam wa miamba na madini kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Abel Sembeka na Bi. Edika Masisi, wameshiriki katika warsha na ukaguzi wa bwawa la topesumu lililopasuka Februari 15, 2025 kwenye mgodi wa kampuni ya Sino Metal Leach Zambia Limited nchini Zambia.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Jiolojia ya Sweden (SGU) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Lulea kutoka nchini Sweden na Chuo Kikuu cha Copperbelt cha nchini Zambia, huku Wizara ya Madini na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira nchini Zambia (ZEMA) wakiwa wenyeji.

Warsha hiyo umehusisha pia wataalam wa migodi na mazingira kutoka nchi za Afrika Magharibi, Mashariki na Kusini mwa Afrika waliopata mafunzo ya usimamizi wa miamba taka na maji migodini kupitia mradi wa ITP 308 chini ya uratibu wa SGU.

Lengo kuu la warsha hiyo ni kutembelea na kufanya tathmini ya bwawa la topesumu lililopasuka, kujifunza chanzo cha tatizo, mbinu bora za usanifu na usimamizi wa mabwawa ya topesumu, pamoja na hatua za kupunguza madhara kwa mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.






NEMC YASHIRIKI WARSHA YA KUJADILI UREJESHWAJI IKOLOJIA YA MATUMBAWE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Warsha ya kujadili namna bora ya urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya matumbawe iliyofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 16-17 Septemba 2025. 

NEMC imewakilishwa na Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC), Dkt. Rose Sallema Mtui, ambaye pia ni Mratibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuhifadhi na kutunza matumbawe. 

Kikao hicho kimeratibiwa na shirika la Uhifadhi Mazingira la “The Nature Conservancy”

Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema akiwasilisha mada katika Warsha hiyo

Baadhi ya washiriki wa Warsha hiyo wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika Warsha hiyo




Baadhi ya wawasilishaji wakiwasilisha mada katika Warsha hiyo


Washiriki wa Warsha ya kujadili namna bora ya urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya matumbawe wakiwa katika picha ya pamoja, Warsha hiyo imefanyika Zanzibar kuanzia tarehe 16-17 Septemba 2025. 

NEMC YASHIRIKI WASILISHO LA RIPOTI YA MAKUNDI MAALUM KUTOKA KWA ASASI YA WATED JIJINI DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeshiriki uwasilishaji wa ripoti ya mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni kwenye sera ya Taifa ya Ardhi 1995 (Toleo la 2023) na mchakato wa NDC 3.0V  uliofanyika katika ukumbi wa Residence Jijini Dodoma leo.

Akiwasilisha ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na WAHEAL na  Tree of Hope, Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia kutoka Women Action Towards Entrepreneurship Development (WATED) Bi. Maria Matui amesema imelenga kuainisha changamoto za wanawake wa vijijini pamoja na kusaidia jitihada za mashirika katika kupaza sauti za wanawake kwenye masuala ya usimamizi wa ardhi na harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Walioshiriki katika uwasilishaji wa ripoti Asasi ya WATED ya mchango wa wanawake, wasichana na makundi wakiwa katika picha ya pamoja .

 
Amesema wasilisho hilo lililohusisha pia wanachama wa mtandao wa mabadiliko ya tabianchi limeainisha changamoto nyingi wanazopitia wanawake wa vijijini zikiwemo, mila na desturi, mitazamo na mifumo dume hali inayoathiri masuala ya maendeleo hasa shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya washiriki wa wasilisho la Asasi ya WATED wakiwa 
 katika ukumbi wa Residence leo Septemba 17, 2025  Dodoma 

Malengo makubwa matatu yaliyowasilishwa ni pamoja na kuweka wazi mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni katika utekelezaji wa Sera ya Ardhi ya 1995(Toleo la 2023, kushirikiana na Serikali katika kuboresha mchakato wa NDC.3.0V kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za makundi yote ya jamii pamoja na kutoa mapendekezo Sera shirikishi yatakayohakikisha usimamizi endelevi wa rasilimali na upatikanaji wa haki sawa kwa kila mmoja.

Baadhi ya washiriki wa wasilisho la Asasi ya WATED wakifuatilia wasilisho hilo lililofanyika  katika ukumbi wa Residence leo Septemba 17, 2025  Dodoma 

Mikoa iliyofikiwa na Asas hizi ni pamoja na Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Geita, Arusha, Mara, Kagera na Tanga.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...