Nyumbani

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗜𝗙𝗨𝗡𝗚𝗜𝗔 𝗞𝗜𝗪𝗔𝗡𝗗𝗔 𝗖𝗛𝗔 𝗦𝗔𝗡 𝗦𝗛𝗔𝗡 𝗡𝗔 𝗕𝗔𝗜-𝗟𝗬 𝗣𝗔𝗣𝗘𝗥 𝗖𝗢. 𝗟𝗧𝗗 𝗠𝗞𝗨𝗥𝗔𝗡𝗚𝗔 𝗞𝗪𝗔 𝗨𝗞𝗜𝗨𝗞𝗪𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗦𝗛𝗘𝗥𝗜𝗔 𝗬𝗔 𝗠𝗔𝗭𝗜𝗡𝗚𝗜𝗥𝗔

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekifungia kiwanda cha SAN SHAN na BAI-LY PAPER CO. LTD kwa kukiuka sheria na taratibu za mazingira, hatua iliyochukuliwa baada ya timu ya ukaguzi wa mazingira uliofanyika katika Wilaya ya Mkuranga ukiongozwa na Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Mhandisi Luhuvilo Mwamila.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Luhuvilo alisema kiwanda cha SAN SHAN kinachojihusisha na uchakataji wa mafuta machafu (waste oil) kimekuwa kikizalisha moshi mzito na harufu kali kutokana na kukosa mfumo wa kudhibiti hewa chafuzi. Aidha, kiwanda hicho kimekuwa kikitiririsha maji taka yenye mafuta machafu kwenye mazingira na kusababisha uchafuzi mkubwa katika maeneo ya jirani.

NEMC imebainisha kuwa kiwanda hicho hakina Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) na kwamba mwekezaji wake amekuwa akiwazuia wakaguzi kutekeleza majukumu yao ya ukaguzi, hali iliyokwamisha juhudi za kitaalamu za kushauri maboresho ya uzalishaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira. NEMC pia ilieleza kuwa viongozi wa Halmashauri walishindwa kukikagua kiwanda hicho kutokana na vikwazo vilivyowekwa na uongozi wa kiwanda.

Kwa upande wa kiwanda cha BAI-LY PAPER CO. LTD, kinachozalisha karatasi za chooni (Toilet paper), kimekutwa kikitiririsha maji taka kwenye mazingira na kusababisha uchafuzi unaohatarisha afya za wakazi wa maeneo ya jirani.

Kutokana na changamoto hizo, NEMC ilishirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha ukaguzi wa viwanda hivyo na hatimaye kuvifungia. Bi. Luhuvilo ametoa rai kwa viwanda vyote nchini kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kushirikiana na wakaguzi ili kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.







NEMC YASHIRIKI KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI-DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika tarehe 5 Juni 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo, yanayofanyika kila mwaka tarehe 5 Juni, kwa mwaka huu yaliadhimishwa kitaifa kwa kauli mbiu isemayo “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”.


Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi ambapo kabla ya kilele cha Maadhimisho hayo kikitanguliwa na maonesho ya wiki nzima yaliyolenga kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira kupitia banda lake maalum.

Katika hafla hiyo pia ulizinduliwa Mkakati wa Kitaifa wa Kukijanisha Tanzania ikiwa ni hatua kufikia Taifa linalostawi kiuchumi bila kuharibu Mazingira.

















NEMC YAMTAMBUA JACKLINE ELIABI KWA WASILISHO BORA LA UCHUMI MZUNGUKO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limemtambua mwanafunzi wa Darasa la Sita, Jackline Eliabi wa Shule ya Msingi Manyinga, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, kwa uwasilishaji wake bora wa dhana ya Uchumi Mzunguko katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.

Jackline alipata pongezi na kutunukiwa zawadi baada ya kuwasilisha kwa umahiri dhana hiyo muhimu inayohamasisha matumizi endelevu ya rasilimali, upunguzaji wa taka na uhifadhi wa mazingira. Uwasilishaji wake ulionesha uelewa mkubwa wa masuala ya mazingira na mchango wa wanafunzi katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu.

Zawadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, ikiwa ni kutambua mchango wa wanafunzi katika kusukuma gurudumu la uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini. Dkt. Semesi alieleza kuwa wanafunzi ni wadau muhimu katika juhudi za kulinda mazingira na kwamba wao ndio mabalozi wa baadaye wa mazingira watakaosaidia kuendeleza agenda ya maendeleo endelevu kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.





DKT. NCHIMBI AZURU BANDA LA NEMC MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Emmanuel Nchimbi ametembelea Banda la NEMC Leo ikiwa ni  siku ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoadhimishwa kila tarehe 5, Mei ya Kila mwaka ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.


Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” ikihamasisha ushiriki wa wadau wote katika kutunza mazingira, kupambana na uharibifu wa mazingira na kuendeleza matumizi endelevu ya rasilimali asilia kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa vizazi vijavyo.





Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (kushoto ) akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Kanda ya Kati (NEMC) Bw. Novatus Mushi, mara baada ya kuzuru Banda la NEMC katika wiki ya Maonesho ya kuelekea Siku ya Mazingira Duniani  yanayofanyika viwanja vya  Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma. Kilele cha Maadhimisho hayo ni tarehe 5 Juni 2026.

𝗠𝗪𝗘𝗡𝗬𝗘𝗞𝗜𝗧𝗜 𝗪𝗔 𝗕𝗢𝗗𝗜 𝗬𝗔 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗔𝗞𝗜𝗠𝗕𝗜𝗔 𝗞𝗜𝗟𝗢𝗠𝗜𝗧𝗔 𝟱

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mhandisi Mwanasha Tumbo, ameshiriki mbio za kilomita 5 zilizofanyika katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. 


Mbio hizo zililenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kuendeleza afya kupitia shughuli za michezo.

Tukio hilo liliwakutanisha viongozi wa Serikali, wadau wa mazingira na wananchi mbalimbali, likibeba ujumbe wa pamoja wa kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.



WAZIRI MASAUNI AZURU BANDA LA NEMC MAONESHO WIKI YA KUELEKEA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni azuru Banda la NEMC wiki ya Maonesho ya kuelekea Siku ya Mazingira Duniani  yanayofanyika viwanja vya  Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma. Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi tarehe 1 Juni 2026 ambapo kilele cha Maadhimisho hayo ni tarehe 5 Juni 2026 huku yakibeba Kaulimbiu "Dira 2050 - Tuwajibike Kukijanisha Tanzania"




𝗨𝗦𝗜𝗠𝗔𝗠𝗜𝗭𝗜 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗭𝗜𝗡𝗚𝗜𝗥𝗔 𝗨𝗘𝗡𝗗𝗘 𝗦𝗔𝗠𝗕𝗔𝗠𝗕𝗔 𝗡𝗔 𝗨𝗞𝗨𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗪𝗘𝗞𝗘𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗡𝗪-𝗠𝗔𝗝𝗜, 𝗠𝗛𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗜 𝗞𝗨𝗡𝗗𝗢 𝗠𝗔𝗧𝗛𝗘𝗪

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew amesisitiza umuhimu wa NEMC kuharakisha mifumo ya mawasiliano na tehama katika kuratibu shughuli za Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) na TISEZA kwenye upangaji wa maeneo ya uwekezaji na kuwataka kuwa na mpango kazi ulio wazi (clear roadmap) utakaoruhusu Tathmini za Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) kufanyika kwa haraka na ufanisi mkubwa, hatua itakayosaidia kuondoa urasimu na kuchochea kasi ya wawekezaji kuleta mitaji yao nchini.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, ameipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ubunifu na mikakati thabiti wakati alipotembelea banda lao katika Maonesho ya Kuelekea Siku ya Mazingira Duniani.



PLASTIKI HAI ILIYOTENGENEZWA KWA MABAKI YA CHAKULA YAWA KIVUTIO MAONESHO KUELEKEA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI

Mfumo wa Plastiki hai ambao ni rafiki kwa Mazingira kutoka chuo kikuu Ardhi wawa kivutio Banda la NEMC Maonesho ya Mazingira kuelekea Siku ya Mazingira Duniani.

Mfumo huu unahusisha magamba ya samaki, mabaki ya vyakula kama magamba ya mihogo, magamba ya ndizi na pumba za mpunga zinachakatwa na kutengeneza Plastiki hai ambazo ni rafiki kwa Mazingira zinazoweza kutumika kama vifungashio







NEMC YATAMBUA MCHANGO WA TFS KAMPENI YA UPANDAJI MITI NCHI NZIMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetambua mchango wa TFS katika zoezi Zima la kampeni ya upandaji miti 40,000 nchi nzima kwa kumpatia zawadi Naibu Kamishna wa Uhifadhi (TFS) Salehe S. Beleko alipozuru Banda la NEMC viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Center ikiwa ni wiki ya Maonesho kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yenye kaulimbiu isemayo Dira 2050- Tuwajibike kukijanisha Tanzania.






"𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗠𝗡𝗔𝗙𝗔𝗡𝗬𝗔 𝗞𝗔𝗭𝗜 𝗡𝗭𝗨𝗥𝗜" -𝗡𝗪-𝗧𝗔𝗠𝗜𝗦𝗘𝗠𝗜, 𝗗𝗞𝗧. 𝗦𝗘𝗜𝗙

Ni kauli yake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), anayeshugulikia Afya, Dkt. Rajabu Seif, alipotembelea banda la NEMC  viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre, Jijini Dodoma kwenye maonesho ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika 05/06 Kila Mwaka ambayo kwa mwaka huu yanakaulimbiu isemayo Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.


Akiwa katika banda hilo, Dkt. Seif alipongeza juhudi za NEMC katika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.

Alisema kazi inayofanywa na NEMC ina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu wajibu wao wa kulinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za asili zinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Katika banda hilo, wananchi wanapata elimu kuhusu umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii, umuhimu wa upandaji miti, utenganishaji wa taka kuanzia kwenye chanzo, pamoja na dhana ya taka sifuri inayolenga kupunguza uzalishaji wa taka na kuongeza matumizi ya mbinu za urejelezaji. 

Dkt. Seif alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya NEMC, taasisi mbalimbali na wananchi ni muhimu katika kufanikisha agenda ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira nchini inafanikiwa kwa maendeleo endelevu.

ELIMU YA MAZINGIRA IKITOLEWA KATIKA MAONESHO YA KUELEKEA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI JUNI 5 2026

 Elimu ya Mazingira ikiendelea kutolewa katika Banda la NEMC katika maonesho kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma 

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi tarehe 1 Juni 2026 na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa.