Nyumbani

NEMC YASHIRIKI KONGAMANO LA PIKA KIJANJA 2025 – UBUNGO PLAZA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo 22 Agosti, 2025 limeshiriki  Kongamano la Pika Kijanja lililoandaliwa na TBC pamoja na Bongo FM ambalo ni sehemu ya Kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia.

Kongamano hilo limefanyika katika Ukumbi wa Ubungo plaza ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila akizungumza katika Kongamano hilo

Akizungumza, mgeni katika Kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam  mhe. Albert Chalamila, amesema jamii ikiendelea kutumia nishati chafu ya kupikia itahatarisha usalama wa vizazi vijavyo kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya nishati hiyo, jambo ambalo ameliita ni usaliti wa dunia ijayo. 

Katika Kongamano hilo NEMC pia imeshiriki majadiliano yaliyolenga kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya Nishati safi ya kupitia ikiwemo gesi na pia kuelimisha kuhusu madhara ya Nishati chafuzi kwa Afya na Mazingira.

Baadhi ya Maafisa wa NEMC katika Kongamano hilo

Kongamano hili lililowakutanisha wadau mbalimbali wa Nishati na Mazingira wakiwemo wanawake linafanyika kwa mara ya tano tangu kampeni ya Pika Kijanja ilipoanzishwa mwaka 2022


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila (wa pili kulia) na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo

𝐁𝐎𝐃𝐈 𝐘𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐍𝐎𝐋𝐄𝐖𝐀 𝐌𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐖𝐀 𝐔𝐅𝐔𝐀𝐓𝐈𝐋𝐈𝐀𝐉𝐈 𝐌𝐀𝐙𝐈𝐍𝐆𝐈𝐑𝐀 𝐊𝐈𝐃𝐈𝐉𝐈𝐓𝐀𝐋𝐈


Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imepitishwa kwenye wasilisho maalum kuhusu Mfumo wa Kidijitali wa Kufuatilia Uchafuzi wa Mazingira ujulikanao kama Online Continuous Emissions Monitoring System (OCEMS).

Mfumo huu wa kisasa umeundwa kwa lengo la kufanikisha ufuatiliaji wa wakati halisi wa viwango vya uchafuzi vinavyotolewa na viwanda na sekta mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika kusimamia mazingira nchini.

Kupitia mfumo huu, taarifa za uchafuzi wa hewa zitapatikana moja kwa moja na kwa wakati  jambo ambalo litasaidia katika kufanya uamuzi sahihi kuhusu hatua za kudhibiti uchafuzi. Aidha, mfumo huu utawezesha kuimarika kwa ushirikiano kati ya wadau wa mazingira kwa kuwa taarifa zitakuwa wazi na zinazopatikana kwa urahisi, hivyo kuchochea jitihada za pamoja katika kulinda mazingira na afya ya jamii.


Bodi ya NEMC ikipatiwa Mafunzo ya mfumo wa ufuatiliaji wa Mazingira Kidigitali

NEMC YAFANIKISHA MAFUNZO YA KUJENGEA UWEZO KITAIFA WIZARA, TAASISI NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA JUU YA NYENZO ZA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza za la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limefanikisha mafunzo ya kujenga uwezo wa kitaifa juu ya nyenzo za Usimamizi wa Mazingira nchini kwa Wizara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za mitaa.

Mafunzo hayo ya siku mbili   yalianza jana 20 Agosti, hadi leo 21, 2025 katika Hoteli ya Midland Jijini Dodoma huku yakihusisha uwasilishaji wa mada na majadiliano, pamoja na maswali na majibu ya papo kwa papo.

Aidha mafunzo hayo yalilenga kuhakikisha Taasisi zote za umma na Mamlaka za Serikali za mitaa zinahakikisha matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake yanatekelezwa ipasavyo


Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC na Mratibu Mkuu wa Mradi wa EMA upande wa NEMC, Bw. Paul Mashaija Kalokola akizungumza katika Mafunzo hiyo

Baadhi ya mada zilizowasilishwa ni pamoja na hali ya udhibiti wa taka za kielekroniki katika miji na manispaa, changamoto na fursa zilizopo katika taka za kielektroniki,  Udhibiti wa madampo haramu, Mpango mkakati wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii pamoja na Kaguzi za Mazingira pamoja na mchakato wa kupata vibali vya taka hatarishi pamoja na changamoto zilizopo katika udhibiti wake. 


Baadhi ya maafisa wa NEMC wakiwasilisha mada katika Mafunzo hiyo

Katika kuhitimisha mafunzo hayo baadhi ya washiriki wamelishukuru Baraza kwa mafunzo hayo huku wakieleza kuwa wamepata mbinu mpya ambazo awali hawakuwa nazo katika swala zima la Usimamizi wa Mazingira nchini.



Baadhi ya washiriki wa Semina hiyo

NEMC YAZITAKA TAASISI ZA UMMA KUTEKELEZA KWA UFANISI SHERIA YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezitaka taasisi za umma zikiwemo Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake yanatekelezwa ipasavyo katika maeneo yao ya kazi.

Wito huo umetolewa leo, tarehe 20 Agosti 2025, katika semina ya mafunzo ya nyenzo za usimamizi wa mazingira chini ya Mradi wa EMA kwa Taasisi za Umma inayoendelea katika Hoteli ya Midland, Jijini Dodoma kuanzia tarehe 20 hadi 21 Agosti 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, mgeni rasmi ambaye ni Meneja wa Maeneo Maalumu na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Careen Anatory Kahangwa, amesema lengo la semina hiyo ni kuimarisha mbinu za kazi na uwezo wa utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, sambamba na kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi kwa ajili ya usimamizi bora wa mazingira nchini.

Meneja wa Maeneo Maalumu na Mabadiliko ya Tabianchi (NEMC), Dkt. Careen Anatory Kahangwa akizungumza wakati wa Semina ya kujenga uwezo wa kitaifa juu ya nyenzo za Usimamizi wa Mazingira nchini kwa Wizara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa chini ya Mradi wa EMA.

"Ushiriki wenu katika kikao hiki ni wa muhimu kwa kuwa unalenga kuhakikisha utekelezaji wa sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa ya mazingira. Hii itawezekana tu iwapo mtayapokea mafunzo haya kwa umakini na kuyazingatia ili kujengewa uwezo wa kutosha katika kusimamia vyema mazingira," alisema Dkt. Kahangwa.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC na Mratibu Mkuu wa Mradi wa EMA, Bw. Paul Mashaija Kalokola ameeleza kuwa kumekuwa na uhitaji mkubwa wa kujengea uwezo taasisi mbalimbali ili wadau waweze kufahamu na kutumia nyenzo muhimu za usimamizi wa mazingira nchini.

Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC na Mratibu Mkuu wa Mradi wa EMA upande wa NEMC, Bw. Paul Mashaija Kalokola akizungumza katika Semina hiyo

Ameongeza kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni udhaifu wa baadhi ya taasisi katika kutekeleza ipasavyo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa mradi huo wa miaka mitatu unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, wenye lengo la kuimarisha uwezo wa wadau wote nchini katika kusimamia mazingira kwa ufanisi.

Baadhi ya washiriki wa semina ya mafunzo ya nyenzo za usimamizi wa mazingira chini ya Mradi wa EMA   





Baadhi ya washiriki wa Semina hiyo wakichangia mada 


Washiriki wa Semina  ya kujenga uwezo kitaifa juu ya nyenzo za usimamizi wa Mazingira chini ya Mradi wa EMA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya awamu ya kwanza ya mafunzo hayo


NEMC YAWATAKA WAMILIKI WA MABASI KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA BARABARANI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri pamoja na abiria kuboresha usafi katika mabasi na maeneo ya usafiri barabarani, kwa kuzuia tabia ya kutupa taka nje ya magari na kukojoa mabarabarani.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokuwa akiongea na vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kusimamia Mazingira nchini. 

Amesema kumekuwepo na mitazamo iliyojengeka kwa abiria wa mabasi makubwa yanayoenda safari ndefu na fupi ya kutokuthamini mazingira na kuwa na tabia ya kutupa taka ovyo na kukojoa barabarani hali inayochafua mazingira, kuharibu hali ya hewa na kuhatarisha afya za jamii. 

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza na vyombo vya Habari wakati akitoa wito wa kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuepuka uchafuzi wa mazingira.

“Mazingira safi ni haki ya kila Mtanzania, na ni jukumu letu sote kuhakikisha tunayahifadhi. Kutupa taka nje ya gari na kukojoa barabarani si tu ni tabia mbaya, bali pia ni ukiukwaji wa Sheria za mazingira. Tunawaomba wasafiri na wamiliki wa mabasi kushirikiana nasi kwa kuweka na kutumia vyombo vya kutupa taka ili tukome uchafuzi huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculate Sware Semesi

Aidha, NEMC imetahadharisha kuwa watakaobainika kutupa taka au kukojoa mabarabarani watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo faini na adhabu nyingine zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria za mazingira.

“Ninawahimiza watanzania wote kuwa mabalozi wa usafi katika maeneo wanayopitia. Tukichukua hatua sasa, tunaweza kulinda afya zetu na mazingira kwa vizazi vya sasa na baadae”.

NEMC imeendelea kutoa simu ya bure 0800 110 115 kwa ajili ya kuripoti uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na abiria, shughuli za binadamu, viwanda bubu au raia ili kuimarisha usimamizi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA KAMATI YA KIMATAIFA GENEVA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limeshiriki Mkutano wa kamati ya kimataifa ya majadiliano ya kuanzisha mkataba wa kimataifa wa kukabiliana na uchafuzi unaotokana na Plastiki nchini nchini Uswisi mjini Geneva

Mkutano huo umehusisha jopo la wadau wa Mazingira kutoka nchini Tanzania likiongozwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) profesa Peter Msofe, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC, TBS, na GCLA ambao walishiriki kikamilifu kwa siku zote kumi za majadiliano ya kuanzishwa Mkataba huo.

Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamadi Taimuru akiwasilisha mada katika Mkutano huo

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msoffe (wa kwanza kulia) na Bw. Hamadi Taimuru (wa pili kushoto) wakifuatilia Mkutano huo


Hata hivyo kutokana na mitazamo na misimamo ya nchi mbalimbali kulingana na maslahi ya nchi zao, majadiliano hayo hayakuweza kufikia muafaka na hivyo mwenyekiti wa Mkutano ndugu Luisaliaghirisha majadiliano mpaka pale atakapotangaza tarehe mpya ya kuendeleza majadiliano hayo na hatimaye kupata mkataba husika.

Majadiliano ya washiriki wa Mkutano huo ikiwa ni sehemu ya Mkutano huo

NEMC YAUNGANA NA TAASISI NYINGINE KUADHIMISHA SIKU MAALUMU YA MAZINGIRA MAONESHO YA SABASABA 2025

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC  Julai 6, 2025  limeungana na Taasisi mbalimbali kuadhimisha Siku ya maalumu ya Mazingira iliyotengwa kwa mara ya kwanza kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba) 2025.

Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo alikuwa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Cyprian Luhemeja huku tukio hilo likibebwa na Kauli mbiu isemayo "Matumizi ya Nishati safi na utunzaji wa Mazingira Kwa ustawi wa Tanzania bora".


Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza wakati wa hafla ya Siku maalumu ya Mazingira iliyotengwa katika maonesho ya Sabasaba 2025 iliyofanyika tarehe 6/7/2025

Akizungumza katika hotuba yake Mhe. Cyprian Luhemeja ameitaka siku hiyo ya tarehe 6 /7 itengwe rasmi kuwa siku maalumu ya Mazingira kila mwaka katika maonesho hayo kuanzia maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa (sabasaba).

Hafla ya Siku maalum ya Mazingira tarehe 6/7/2025 iliyotengwa katika msimu wa maonesho ya Sabasaba 2025

Sambamba na hilo amesisitiza watanzania wote kutunza Mazingira kwa kuwa Mazingira yaliumbwa kwanza Kisha mwanadamu akaumbwa baadae ili ayatunze, ayahifadhi na kuyalinda.

"Hii duniani ilianza kwa kutengenezewa Mazingira, mwanadamu ameumbwa wa mwisho baada ya Mazingira kutengenezewa na mwanadamu alipoumbwa alipewa kazi ya kuyatunza na kuyahifadhi Mazingira lakini mwanadamu anayaharibu kwa uchafuzi na ukataji wa miti.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Bi. Mwanasha Tumbo (wa pili kulia) Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa  Tantrade, Dkt. Latifa M. Khamis (wa tatu kulia), timu ya wanawake na Samia na baadhi ya washiriki wa Siku maalumu ya Mazingira iliyotengwa katika msimu wa maonesho ya Sabasaba 2025

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza washindi wa Mazingira Challenge iliyofanyika siku kadhaa zilizopita ambayo ililenga kumpata balozi kinara wa  Utunzaji wa Mazingira na anayehamasisha utunzaji wa Mazingira kwa kupiga picha ya Mazingira safi yanayomzunguka na kuwasilisha NEMC Kwa ajili ya mashindano hayo.

Maadhimisho hayo yalipambwa na mabalozi wa Mazingira pamoja na watumbuizaji nguli akiwemo Mrisho Mpoto pamoja na Mr. Tree na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC, TANTRADE, STAMICO, Wanawake na Samia, Shirika la PUMA pamoja na wananchi waliotembelea maonesho ya sabasaba.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akimkabidhi zawadi na cheti cha heshima Mshindi wa kwanza wa mashindano ya ‘Mazingira Challenge’ Bw. Paulo Dotto Masele yaliyofanyika katika msimu wa sabasaba

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akimkabidhi zawadi na cheti cha heshima Mshindi wa pili wa mashindano ya ‘Mazingira Challenge’ Bi. Magdalena Chuma yaliyofanyika katika msimu wa sabasaba


Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akimkabidhi zawadi na cheti cha heshima Mshindi wa tatu wa mashindano ya ‘Mazingira Challenge’ Bw. Stanley Urassa  yaliyofanyika katika msimu wa sabasaba

"Hii duniani ilianza kwa kutengenezewa Mazingira, mwanadamu ameumbwa wa mwisho baada ya Mazingira kutengenezewa na mwanadamu alipoumbwa alipewa kazi ya kuyatunza na kuyahifadhi Mazingira lakini mwanadamu anayaharibu kwa uchafuzi na ukataji wa miti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza washindi wa Mazingira Challenge iliyofanyika siku kadhaa zilizopita ambayo ililenga kumpata balozi kinara wa  Utunzaji wa Mazingira na anayehamasisha utunzaji wa Mazingira kwa kupiga picha ya Mazingira safi yanayomzunguka na kuwasilisha NEMC Kwa ajili ya mashindano hayo.

Maadhimisho hayo yalipambwa na mabalozi wa Mazingira pamoja na watumbuizaji nguli akiwemo Mrisho Mpoto pamoja na Mr. Tree na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC, TANTRADE, STAMICO, Wanawake na Samia, Shirika la PUMA pamoja na wananchi waliotembelea maonesho ya sabasaba.



Ugawaji wa Zawadi kwa Wadau wengine 


NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...