Nyumbani

NEMC KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YAENDESHA MAFUNZO YA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA, NJOMBE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia ofisi yake ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wametoa Mafunzo ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa Viongozi na Kamati za Mazingira za Wanawake na Samia katika Mkoa wa Njombe.  

   

Mafunzo hayo yamelenga kupata Wadau na Mabalozi wazuri watakao saidia kusimamia, kutunza na kuelimisha wananchi na jamii kwa ujumla maswala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira katika Mkoa wa Njombe 

Elimu iliyotolewa ni pamoja na Umuhimu wa kutunza Mazingira na faida zake, Umuhimu wa Kutumia Nishati safi ya Kupikia na faida zake.

Kupitia mafunzo hayo, NEMC imewafahamisha washiriki wa mafunzo changamoto nane za kimazingira zilizoainishwa katika Sera ya Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2021 ambazo ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi,  Uharibifu wa Ardhi, Uharibifu wa Misitu, Uharibifu wa Vyanzo vya Maji na kupelekea uhaba na maji yenye ubora mijini na vijijini.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA BIOANUAI, PANAMA 2025

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Utekelezaji wa Mkataba wa Bioanuai unaoendelea Jijini Panama kuanzia tarehe 20 hadi 30 Novemba 2025. 

Tanzania, ikiwa ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Bioanuai (Convention on Biological Diversity – CBD), imeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya bioanuai. Mkutano huu unafanyika katika Ukumbi wa Atlapa Convention Center na unahusisha mikutano miwili mikubwa: SABSTTA-27, inayojadili masuala ya kisayansi, kiufundi na kiteknolojia kuhusu bioanuai; na SB8J-1, inayohusiana na haki na mchango wa jamii za wenyeji katika hifadhi ya bioanuai.

Kupitia ushiriki wake, NEMC imeungana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (TFS na TAWA), pamoja na Shirika la The Nature Conservancy (TNC). Majadiliano katika mikutano hii yamejikita kwenye utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai (Kunming–Montreal Global Biodiversity Framework – KMGBF) uliopitishwa mwaka 2022, yakilenga kuweka miongozo ya kuboresha sera, sheria na programu za kitaifa kuhusu hifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili. 

Aidha, mada kuu zinazojadiliwa ni pamoja na bioanuai na mabadiliko ya tabianchi, bioanuai na afya, viumbe vamizi, bioanuai na kilimo, pamoja na tathmini za athari za viumbe hai vilivyobadilishwa kijenetiki (LMOs).

Kwa Tanzania, ushiriki huu ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na mataifa mengine kuhusu njia bora za kudhibiti upotevu wa bioanuai na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia jukwaa hili, NEMC inaimarisha nafasi yake katika kuunganisha taaluma, sayansi, na jamii katika utekelezaji wa KMGBF, sambamba na kuandaa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji bora wa sera za mazingira nchini.

Vilevile, majadiliano haya yanatoa nafasi ya kuandaa msimamo wa pamoja wa kikanda kuelekea Mkutano wa 17 wa Mkataba wa Bioanuai utakaofanyika Jijini Yerevan, Armenia mwaka 2026.

Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika mkutano huu ni ushahidi wa dhamira ya Tanzania katika kulinda mazingira na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za asili. Unasisitiza kuwa uhifadhi wa bioanuai ni nyenzo muhimu katika kulinda afya ya jamii, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha usalama wa chakula. 

NEMC inaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuhakikisha malengo ya kimataifa ya bioanuai yanatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa na dunia kwa ujumla.

𝗞𝗔𝗠𝗜𝗦𝗛𝗡𝗔 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗞𝗪𝗔 𝗨𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗙𝗨 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔 𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗠𝗠𝗔

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao na watumishi wa NEMC alipozuru Ofisi za Baraza 23 Oktoba, 2025 ikiwa ni ziara yake ya kikazi

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  kwa kuendelea kuonesha uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini.

Akizungumza leo 23 Oktoba, 2025 jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi  ofisi za Baraza  Dkt. Laurean Ndumbaro amesema uadilifu uliooneshwa na Baraza hilo ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine za Umma katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa kikao hicho kilichokuwatanisha watumishi wa Baraza na Ugeni kutoka Tume ya Utumishi wa Umma ukiongozwa na Kamishna Dkt. Laurean Ndumbaro. 

Amesisitiza kuwa uadilifu ndio nguzo kuu ya utumishi wa umma na ndio msingi wa kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi.

Ameongeza kuwa mafanikio ya NEMC katika utekelezaji wa miradi ya kimazingira pamoja na usimamizi wa Sheria na Kanuni za Mazingira ni ushahidi kwamba viongozi na watumishi wake wameweka maslahi ya Taifa mbele kuliko  maslahi binafsi.

Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa akizungumza wakati wa kikao hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amemshukuru  Kamishna kwa Tathmini hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu zaidi kwani pongezi hizo ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika ziara yake Kamishna Dkt. Ndumbaro ameambatana na wataalamu wengine akiwemo Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akimkabidhi zawadi Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya kikao hicho.




   Baadhi ya watumishi wa Baraza wakifuatilia kikao hicho


NEMC NA MWAKILISHI KUTOKA ULAYA WAJADILI NA MJUMBE KUTOKA ULAYA USIMAMIZI WA MAZINGIRA KATIKA SEKTA YA MADINI


Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii Bi. Lilian Lukambuzi (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na muwakilishi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Meneja wa Programu (Utawala wa kiuchumi) Bw. Sebastian Schaber. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Meneja wa Mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (NEMC) Mha. Luhuvilo Mwamila. Wa kwanza kulia ni Meneja Usajili wa Wataalam elekezi wa Mazingira (NEMC) Bi. Edika Masisi. 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na muwakilishi wa ujumbe wa Umoja wa nchi za Ulaya (EU) nchini Tanzania na kujadili namna Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii zinavyofanyika kwa Tanzania na jinsi wanavyoweza kushirikiana na Baraza hususani katika masuala ya kimazingira kwa upande wa Sekta ya madini hasa madini muhimu (Critical Minerals) 

Kikao hiki kilijadili miongozo iliyopo  na kuainisha maeneo yanayohitaji usaidizi wao ili kuwezesha uzingatiaji wa Sheria kwa miradi ya madini inayowekezwa nchini.


NEMC NA IUCN WAJADILI NAMNA YA KUKABILIANA NA UCHAFUZI WA PLASTIKI UKANDA WA BAHARI

Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema akizungumza wakati wa kikao kazi hicho

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) limefanya kikao kazi kujadili namna bora ya kukabiliana na tatizo la uchafuzi unaotokana na taka za plastiki katika ukanda wa bahari. Kikao hicho kimekusudia kuweka mikakati endelevu ya kudhibiti matumizi na utupaji holela wa plastiki, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya baharini kwa manufaa ya viumbe vya majini na ustawi wa binadamu kwa ujumla.






NEMC YAWANOA MAAFISA FORODHA KIGOMA - ELIMU YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa Forodha katika kituo cha mpakani cha Kigoma, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa programu ya kujenga uelewa kuhusu usimamizi wa bidhaa hatarishi kwa mazingira zinazovuka mipaka.


Akifungua mafunzo hayo Oktoba 20, 2025 katika ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Meneja wa Bandari Kigoma Bw. Edward Mabula amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi mbalimbali katika kulinda mazingira na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizo rafiki kwa mazingira.

“Ushirikiano baina ya taasisi kama NEMC, TRA, TPA, TBS, TMDA na wadau wengine ni muhimu sana katika kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini haziwezi kuathiri mazingira yetu,” amesema Bw. Mabula.


Kwa upande wa wawakilishi kutoka NEMC, wameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191.

Aidha, wamefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Forodha ili waweze kutambua mapema bidhaa hatarishi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu inayoendeshwa na NEMC katika vituo vya mipakani vya Mtukula, Rusumo, Kigoma na Tunduma, ikilenga kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia au kutoka nchini zinakidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Washiriki wa mafunzo ya Usimamizi wa Bidhaa hatarishi mipakani wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mafunzo hayo





NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA TEKNOLOJIA ZA UREJESHAJI MAZINGIRA NCHINI AUSTRIA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikao cha kutathmini mapungufu na changamoto za teknolojia za kimazingira zinazotumika kwenye kurejesha mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa (remediation technologies).

Afisa Mazingira Mwandamizi Bi. Kuruthumu Shushu (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Kikao hicho kilifanyika katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA) yaliyopo jijini Vienna, Austria kuanzia tarehe 13-17 Oktoba, 2025.

Lengo la kikao ni kukutanisha wawakilishi kutoka nchi mbalimbali wanaohusika na Udhibiti na Tafiti katika Sekta ya Nishati ya nyuklia ili kujadili njia bora za urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa.

Njia mbalimbali za urejeshaji wa mazingira zilijadiliwa na nchi wanachama pamoja na mapungufu na changamoto zake na kujifunza njia bora inayoweza kutekelezwa na nchi husika.

Uwasilishaji wa mada ukifanyika katika kikao cha kutathmini mapungufu na changamoto za teknolojia za kimazingira zinazotumika kwenye kurejesha mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa (remediation technologies) kilichofanyika nchini Austria 

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...