Nyumbani

NEMC YAHIMIZA SOKO LA KABONI LENYE UADILIFU KWA MAENDELEO ENDELEVU YA TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi, anasisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa miradi ya kaboni ili kuhakikisha inalinda mazingira, inavutia uwekezaji na kuwanufaisha wananchi.

Akishiriki katika Mkutano wa Carbon Market Africa Summit 2026, uliofanyika Kigali Rwanda, Mkurugenzi Mkuu anasisitiza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza soko la kaboni kupitia uhifadhi wa misitu, mikoko, mifumo ikolojia ya bahari, urejeshaji wa ardhi na usimamizi bora wa taka.

NEMC ina jukumu muhimu katika usimamizi wa mazingira na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa matakwa ya mazingira katika miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi ya kaboni, kwa mujibu wa sheria na mamlaka yake.

NEMC inahimiza uwazi, uwajibikaji, ufuatiliaji wa matokeo ya kimazingira na ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha kuwa miradi ya kaboni inachangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi bila kuathiri haki na maslahi ya wananchi.

“Soko la kaboni linapaswa kuwa fursa ya kulinda mazingira, kuvutia uwekezaji wa kijani na kuboresha maisha ya wananchi. Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila mradi unazingatia sheria, unalinda mifumo ikolojia na kuleta manufaa yanayopimika kwa jamii.”


Kupitia usimamizi madhubuti wa mazingira, NEMC itaendelea kutekeleza wajibu wake katika kujenga mazingira wezeshi kwa uwekezaji endelevu na kuchangia maendeleo ya kijani nchini Tanzania.

#Carbonmarketssummit #ofisiyamakamuwarais #marketafricasummit2026 #greeneconomy #circulareconomy

 

 

TANZANIA GREEN SUMMIT YATAMBUA MCHANGO WA NEMC KONGAMANO LA 2026

𝗬𝗮𝗺𝗽𝗮𝘁𝗶𝗮 𝗠𝗸𝘂𝗿𝘂𝗴𝗲𝗻𝘇𝗶 𝗠𝗸𝘂𝘂 𝗧𝘂𝘇𝗼 𝘆𝗮 𝗛𝗲𝘀𝗵𝗶𝗺𝗮 𝗻𝗮 𝗖𝗵𝗲𝘁𝗶 𝗸𝘂𝗳𝗮𝗻𝗶𝗸𝗶𝘀𝗵𝗮 𝗞𝗼𝗻𝗴𝗮𝗺𝗮𝗻𝗼 𝗵𝗶𝗹𝗼

Taasisi ya Grina Foundation imetambua mchango wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kufanikisha Kongamano la Tanzania Green Summit 2026 na kumpatia Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Immaculate Sware Semesi tuzo ya heshima na cheti.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua nafasi yake na NEMC kwa ujumla kama Mlezi wa Tanzania Green Summit na mchango wake katika kufanikisha Kongamano hilo.

 

Shukrani hizo zimewasilishwa leo, Oktoba 7, 2026,  kwa niaba ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Grina Foundation, Bw. Redemptus Caesar Alphonce ambayo ndiyo mratibu mkuu wa Tanzania Green Summit.

 

Akizungumza na wajumbe hao mara baada ya kupokea tuzo hiyo na cheti, Dkt. Semesi ameeleza kuwa Tanzania green summit ni fursa muhimu kwa vijana, wajasiriamali, wafanyabiashara, watunga sera na viongozi kukutana na kujadili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na fursa za ajira na uwekezaji zilizopo kwenye Mazingira.

Aidha, ameipongeza Grina Foundation na waandaaji wote wa Tanzania Green Summit kwa kufanikisha Kongamano hilo huku akiwataka kufanya Maandalizi mapema kwa ajili ya Kongamano hilo mwakani ili kuongeza tija na ufanisi Kongamano hilo.

 

Kongamano la Tanzania Green Summit 2026 limeendelea kuwa sehemu ya mijadala inayolenga kuongeza uelewa na kuhamasisha hatua za pamoja katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kutambua fursa za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira.

 

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akiwa ameshika Tuzo ya heshima na Cheti mara baada ya kukabidhiwa na wajumbe kutoka Grina Foundation ikiwa ni kutambua mchango wake katika kufanikisha Kongamano la Tanzania Green Summit 2026

 

Grina Foundation ni mratibu mkuu wa Kongamano la Tanzania Green Summit ambalo lilifanyika Septemba 15 na 16 likiwakutanisha vijana, wafanyabiashara, wajasiriamali, watunga sera na Viongozi kujadili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na fursa za ajira na uwekezaji zilizopo kwenye Mazingira.

#nemc

#tanzaniagreensummit

@tanzaniagreensummit

WAZIRI MASAUNI AAGIZA KUIMARISHWA KWA USAFI NA USIMAMIZI WA TAKA MTO NG’OMBE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ametoa wito kwa Viongozi wakiwemo wa Halmashauri na NEMC kushirikisha wananchi kikamilifu katika kupanga na kusimamia mifumo ya ukusanyaji taka, elimu ya usafi wa mazingira kuimarishwa na Sheria  kusimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha mazingira ya Mto Ng’ombe yanakuwa safi na salama.

Waziri Masauni ametoa maagizo hayo Oktoba 11, 2026, wakati wa ziara ya kikazi katika eneo la Mto Ng’ombe, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua hali ya mazingira na kuimarisha usimamizi wa taka.

Aidha, Mhe. Masauni amesisitiza umuhimu wa kuendeleza zoezi la usafi wa mazingira, ikiwemo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ili kujenga utamaduni wa usafi na uwajibikaji miongoni mwa wananchi.

Vilevile, ameelekeza hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya wanaokiuka Sheria na Kanuni za mazingira, wakiwemo wakandarasi wa ukusanyaji taka wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Waziri Masauni amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa juhudi zake za kulinda mazingira, huku akihimiza ushirikiano kati ya baraza hilo, wananchi, mamlaka za serikali za mitaa na wadau wengine katika kuboresha usimamizi wa taka kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.








NEMC YASHIRIKI KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA UMOJA WA ULAYA NA TANZANIA

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilishiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania lililofanyika kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 6 Oktoba 2026 nchini Finland, Italia, Uholanzi na Ubelgiji. Kongamano hilo liliwakutanisha wawakilishi wa Serikali, taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara kujadili fursa za biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali, zikiwemo madini, kilimo, TEHAMA na bandari.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uchumi mzunguko (Circular Economy), Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), pamoja na usimamizi wa taka zinazotokana na shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini muhimu (Critical Minerals), vifaa vya umeme na kielektroniki. NEMC ilishiriki katika mijadala ya jopo nchini Finland na Uholanzi kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini muhimu na vipaumbele vya kimkakati vya Tanzania.

Katika mijadala hiyo, NEMC ilieleza umuhimu wa kuzingatia masuala ya ESG, matakwa ya kimazingira na ufuatiliaji wa mnyororo wa thamani wa madini. Ilisisitizwa kuwa uzingatiaji wa viwango hivyo unaweza kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuongeza uaminifu wa wawekezaji.

Aidha, NEMC ilieleza kuwa usimamizi madhubuti wa mazingira na utekelezaji wa kanuni za ESG ni muhimu katika kuvutia uwekezaji endelevu, kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini na kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na shughuli za uchimbaji na uchakataji.

Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika kongamano hilo uliwezesha kubadilishana uzoefu na wadau wa kimataifa na kuwasilisha nafasi ya usimamizi wa mazingira katika kukuza uwekezaji endelevu. Pia, ulitoa fursa ya kuonesha namna uzingatiaji wa masuala ya mazingira, ESG na uchumi mzunguko unavyoweza kuchangia katika kuongeza thamani ya rasilimali za Tanzania na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

 

 



NEMC YATUMIA COP12 KUIMARISHA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA FURSA ZA USHIRIKIANO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki kikamilifu katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika tarehe 6 hadi 9 Oktoba 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Tanzania. Mkutano huo unaofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi umebeba kaulimbiu “Towards Sustainable Blue Economy in the Western Indian Ocean Region for People and Nature: A Journey of Forty Years.”

Ushiriki wa NEMC unaakisi jukumu lake la kisheria na kitaalamu katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa uchafuzi, tathmini ya athari za kimazingira, uzingatiaji wa viwango vya mazingira na ulinzi wa mifumo ikolojia ya bahari na pwani. Kupitia COP12, NEMC inawakilisha masuala ya mazingira ya Tanzania katika majadiliano ya kikanda kuhusu uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuai na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Aidha, NEMC inatumia jukwaa hilo kuimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kubadilishana uzoefu, utaalamu na teknolojia katika usimamizi wa mazingira. Ushirikiano huo ni muhimu katika

Kwa NEMC, COP12 ni fursa muhimu ya kujenga na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, hususan katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.




 

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA FEDHA ZA TABIANCHI (CLIMATE FINANCE)

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika Mkutano wa majadiliano kuhusu Fedha za Tabianchi (Climate Finance Roundtable) uliofanyika tarehe 5 Oktoba 2026 katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam.

Mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo, sekta ya fedha na sekta binafsi kujadili namna ya kuongeza upatikanaji na uhamasishaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza uchumi wenye ustahimilivu.

Majadiliano yamejikita pia katika kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuandaa miradi ya tabianchi inayoweza kufadhiliwa, pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huu umefanyika katika wakati muafaka ambapo Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa zinaendelea na maandalizi kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) utakaofanyika mwezi Novemba 2026 jijini Antalya, Türkiye. Hivyo, majadiliano haya yanatoa fursa muhimu ya kuimarisha vipaumbele vya Tanzania katika eneo la fedha za tabianchi na kuendeleza mikakati ya kuvutia rasilimali zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ushiriki wa NEMC katika mkutano huo unaendeleza mchango wa Baraza katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi, uandaaji na usimamizi wa miradi ya tabianchi, pamoja na jitihada za kuongeza upatikanaji wa fedha za kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

 

 

NEMC KANDA YA BAGAMOYO YASHIRIKI UZINDUZI WA "BALOZI BATILDA ENVIRONMENT DAY"

NEMC Kanda ya Bagamoyo imeshiriki uzinduzi wa ' Balozi Batilda Environment Day' inayolenga kuhakikisha usafi wa mazingira unakuwa sehemu ya maisha ya kila siku, uzinduzi huo umefanyika Oktoba 3, 2026 huku ukimbatana na zoezi la usafi lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa  Balozi Dkt Batilda Burian katika eneo la Tangamani Jiji la Tanga. Katika zoezi hili NEMC imetoa cheti cha pongezi kwa Ndugu Mohamed Ally Hilali kwa kutambua mchango wake katika utunzaji wa mazingira na Usafi Jiji la Tanga.











NEMC YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kujadili utekelezaji wa baj...