Nyumbani

NEMC YASHIRIKI WARSHA YA MAPITIO YA RASIMU YA UHIMILIVU DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Warsha ya Wadau inayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 17 hadi 20 Agosti 2026. Warsha hiyo imeandaliwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa Barabara kwa Ujumuishaji na Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE).

Warsha hiyo inalenga kufanya mapitio na uboreshaji wa Rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi (NCCR-AP) pamoja na Miongozo ya Utekelezaji kwa Sekta ya Barabara nchini Tanzania.

Lengo kuu la warsha ni kukusanya maoni na michango kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuboresha nyaraka hizo na kuhakikisha zinatoa mwongozo madhubuti wa kuimarisha uhimilivu wa miundombinu ya barabara dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.

NEMC YAUNGA MKONO MAAGIZO YA MKUU WA MKOA KUHUSU TAKA SIFURI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, kuhusu utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Kata za Chamazi na Toangoma, Meneja wa Kanda ya Temeke wa NEMC, Bw. Abel Sembeka, alisema NEMC inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutenganisha taka katika chanzo na kuhakikisha taka zinazoweza kurejelezwa, kama plastiki, karatasi, vyuma na vioo, zinakusanywa na kupelekwa kwa wachakataji badala ya kutupwa ovyo.

Ameongeza kuwa maagizo hayo yanaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama na endelevu, huku jamii ikihamasishwa kupunguza uzalishaji wa taka, kutenganisha taka katika vyanzo na kuimarisha urejelezaji wa taka ili ziweze kutumika tena kama malighafi na fursa ya kiuchumi ndani ya mzunguko wa uchumi wa kijani

NEMC imeahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Temeke na wadau wengine wa Mazingira katika kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri, hususan katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu urejelezaji na matumizi ya taka kama rasilimali, kwa lengo la kupunguza taka zinazopelekwa dampo na kujenga Dar es Salaam safi na yenye mazingira endelevu.












NEMC KANDA YA KUSINI YATOA ELIMU YA UHIFADHI WA MAZINGIRA - MTWARA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kanda ya Kusini limetoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, tarehe 15 Agosti 2026, kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, wajibu wa jamii katika uhifadhi wa mazingira na fursa za kiuchumi zinazotokana na usimamizi endelevu wa mazingira katika Mkoa wa Mtwara na mikoa jirani.

Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi kupitia Dira Mpya Group na Star Women, vikundi vinavyojishughulisha na usafi wa mazingira na ujasiriamali. Mafunzo hayo yameongozwa na Meneja Ngowo Gift, akishirikiana na Dkt. Kharid Mwakoba na Obasanjo Nniwako kutoka NEMC.


Katika mafunzo hayo, wananchi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira, sambamba na kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na matumizi na usimamizi endelevu wa rasilimali za mazingira.

Katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi ni Nguzo ya Tatu ya Dira hiyo. Hivyo, mazingira si suala la pembeni katika maendeleo ya Taifa, bali ni sehemu ya msingi ya Tanzania tunayoijenga kwa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.

Juhudi za utoaji wa elimu ya mazingira zinazoendelea kufanywa na NEMC zinalenga kujenga jamii yenye uelewa na uwezo wa kutambua athari za uharibifu wa mazingira, kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti madhara, pamoja na kutumia fursa zinazotokana na usimamizi endelevu wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

NEMC inaendelea kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, kwa kutambua kuwa mazingira salama ni msingi wa afya, maendeleo na uchumi endelevu wa Taifa







NKM OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA) DKT. MADUHU KAZI AZURU NEMC

Aipongeza Serikali kwa kuthamini Mazingira katika Dira ya 2050 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Maduhu Kazi, amezuru NEMC kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kushika wadhifa huo

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kazi ameipongeza Serikali kwa kuthamini masuala ya Mazingira na kuipa kipaumbele ajenda ya mazingira katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo ya Taifa yanaenda sambamba na uhifadhi endelevu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, ameipongeza NEMC kwa uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake na kulitaka Baraza kuendelea kusimamia misingi ya Sheria, huku likiimarisha ufanisi katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa na vizazi vya baadae.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokuwa akizungumza alimweleza Dkt. Kazi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Baraza na hatua zinazochukuliwa katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira, huku akiahidi kuendelea kusukuma mbele ajenda ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuzingatia Sheria, Kanuni  na miongozo ya Serikali.














NEMC YAONGEZA VYOMBO VYA USAFIRI KUIMARISHA MIUNDOMBINU WEZESHI YA UTEKELEZAJI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeongeza vyombo vya usafiri kwa kutumia mapato yake ya ndani, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha miundombinu wezeshi ya utekelezaji wa majukumu ya kimazingira, ikiwemo ufuatiliaji, ukaguzi na uzingatiaji wa Sheria ya mazingira nchini.

Akizungumza leo Agosti 11, 2026 wakati wa makabidhiano ya magari mawili kwa baadhi ya viongozi wa Baraza, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema Baraza limeanza na magari mawili kati ya matano kwa ajili ya viongozi na linatarajia kununua magari mengine 20 ndani ya mwaka huu kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi katika Kanda zote 13 nchini.


 
“Magari haya tumeyanunua sisi wenyewe kwa kutumia mapato yetu ya ndani na tunaanza na magari 5 kwa ajili ya viongozi, lakini kwa malengo tuliyojiwekea kwa mwaka huu tutanunua magari mengine 20 " amesema Dkt. Semesi.

Ameongeza “Hii ni katika kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi katika jukumu tulilokasimiwa la usimamizi wa mazingira nchini, sawa na malengo na matakwa ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na malengo ya Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,”

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Bw. Dickson Mjinja alipozungumza aliahidi utunzwaji wa magari hayo na kutumika kwa malengo kusidiwa huku akisistiza uwajibikaji kufikia





NEMC YAWEKA MSINGI WA UTEKELEZAJI WA ESG NA URIPOTI WA UENDELEVU


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuimarisha uwezo wake katika masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (Environmental, Social and Governance – ESG) pamoja na uripoti wa uendelevu, kupitia mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na KPMG kuanzia tarehe 3 hadi 7 Agosti 2026 katika Ofisi ya Kanda ya Temeke ya NEMC, Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango endelevu wa Baraza wa kuimarisha mifumo na kanuni za ESG na kuweka uripoti wa uendelevu kuwa sehemu ya utendaji wa kitaasisi. Mpango huo unahusisha maandalizi ya Sera ya ESG, Mfumo wa ESG, pamoja na Ripoti ya Uendelevu ya Baraza kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa na mifumo ya kimataifa inayotambulika katika uripoti wa uendelevu.


Katika mafunzo hayo, maafisa walioteuliwa kuwa Mabingwa wa ESG na Uripoti wa Uendelevu (ESG & Sustainability Reporting Champions) walipata uelewa na ujuzi wa vitendo kuhusu misingi ya ESG, mifumo ya uripoti wa uendelevu, tathmini ya masuala muhimu ya kimazingira, kijamii na kiutawala, ushirikishwaji wa wadau, usimamizi wa takwimu za ESG, pamoja na namna ya kuandaa na kuratibu uripoti wa uendelevu ndani ya taasisi.


Aidha, mafunzo hayo yameweka msingi wa kuanza kwa vikao na shughuli za vitendo vitakavyowezesha maandalizi ya Sera ya ESG, Mfumo wa ESG na Ripoti ya kwanza ya Uendelevu ya NEMC. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa masuala ya ESG yanaendelea kujumuishwa katika mipango, shughuli na mifumo ya utendaji wa Baraza.


Kupitia hatua hiyo, NEMC inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira, ufanisi wa kitaasisi, uwajibikaji na uwazi, sambamba na kuchangia katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na vipaumbele vya taifa.




MKUTANO WA 48 WA KAMATI YA URITHI WA DUNIA WA UNESCO WAHITIMISHWA RASMI BUSAN, JAMHURI YA KOREA

Tarehe 29 Julai 2026, ulihitimishwa rasmi Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia wa UNESCO (48th Session of the World Heritage Committee) uliofanyika jijini Busan, Jamhuri ya Korea, ukihusisha wajumbe kutoka Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 pamoja na wadau mbalimbali wa kimataifa.

Mkutano huo ulitoa fursa ya kujadili na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya maeneo ya Urithi wa Dunia. Aidha, ulijadili hali ya uhifadhi wa maeneo yaliyopo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia, mapendekezo ya maeneo mapya ya kuorodheshwa, pamoja na changamoto zinazoathiri urithi wa asili na wa kiutamaduni duniani, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la shughuli za kibinadamu.

Tanzania ilishiriki kikamilifu katika mkutano huo, ikichangia mijadala kuhusu uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia, usimamizi wa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuwai na matumizi ya mbinu za kisayansi katika kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira. Ushiriki huo umeendelea kuonesha dhamira ya nchi katika kutekeleza Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi wa urithi wa asili na wa kiutamaduni.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha maeneo ya Urithi wa Dunia nchini yanalindwa na kusimamiwa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira.

Kupitia ushiriki katika majukwaa ya kimataifa kama haya, Tanzania inaendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu na mataifa mengine, huku ikiimarisha nafasi yake katika juhudi za pamoja za kulinda urithi wa dunia na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa ...