Nyumbani

 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo tarehe 26, Septemba, 2025 limefanya Kikao na wadau kutoka Benki ya Dunia ili kujadili fursa za mazingira zinazoweza kuchangia katika uongezaji wa thamani kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Majadiliano hayo yaliyoongozwa na Meneja wa NEMC-Kanda ya Ziwa Magharibi Bw. Boniface Guni ambayo yalilenga kutambua kwa ujumla majukumu ya NEMC na vipaumbele vyake katika sekta ya Madini.

Meneja wa NEMC-Kanda ya Ziwa Magharibi Bw. Boniface Guni (kulia) akizungumza katika Kikao hicho

Wataalamu kutoka Benki ya Dunia wakiwa katika Kikao hicho kilichofanyika tarehe 26, Septemba, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa NEMC Jijini Dar es Salaam

NEMC YAADHIMISHA SIKU YA AFYA MAZINGIRA DUNIANI, ELIMU YA MAZINGIRA YATOLEWA SHULENI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuadhimisha Siku ya Afya mazingira Duniani, Leo tarehe 26 Septemba limetembelea  Shule ya Msingi Mikocheni "A" na kutoa elimu ya Afya na Mazingira kwa wanafunzi na walimu ambapo kaulimbiu kwa mwaka huu 2025 ni "Tokomeza taka za plastiki, Jenga jamii yenye afya Bora.

Elimu hiyo imejikita katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira shuleni, pamoja na kuelezea Dhana ya Punguza, Tumia tena na Rejeleza katika Udhibiti wa taka ikiwa ni pamoja na kufundisha kuhusu usafi wa mwili na mazingira ya nyumbani. 

Afisa Mazingira wa NEMC Bi. Rukia Ally akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni "A" katika Maadhimisho ya Siku ya Afya Mazingira Duniani tarehe 26, Septemba.

Wanafunzi walishirikiana kwa kuuliza maswali na kujifunza mbinu rahisi za kuhakikisha mazingira yao yanabaki safi na salama kwa wote.

Aidha, maafisa hao walitoa wito kwa jamii nzima kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kulinda mazingira, kwani afya njema haiwezi kupatikana endapo mazingira yanaharibika. Waliwataka wazazi, walimu na viongozi wa jamii kuhakikisha elimu hiyo inapelekwa hadi majumbani na maeneo ya kazi, ili kila mmoja awe balozi wa mazingira bora.

Hivyo basi, maadhimisho ya Siku hii yamekuwa chachu ya kuimarisha mshikamano wa pamoja katika kuyalinda mazingira kwa mustakabali endelevu wa kizazi cha sasa na kijacho.

Maafisa wa NEMC wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni A mara baada ya kutoa elimu ya Mazingira kwa wanafunzi wa Shule hiyo ikiwa ni sehemu ya Kuadhimisha Siku ya Afya Mazingira Duniani

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni A wakifuatilia Elimu iliyotolewa na Maafisa Mazingira kutoka NEMC katika Maadhimisho ya Siku ya Afya Mazingira Duniani

PICHA ZA MATUKIO KATIKA KONGAMANO LA UNESCO LA PROGRAMU YA BINADAMU NA HIFADHI HAI CHINA


NEMC na TANAPA katika Kikao cha Kimataifa cha Kamati ya Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai kinachofanyika jijini Hangzhou nchini China kuanzia tarehe 26-28 Septemba 2025. Pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Dkt. Immaculate Sware Semesi (Kulia) na Meneja wa Tafiti za Mazingira, Dkt. Rose Sallema na Mr. Albert Mziray Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TANAPA
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kushoto) katika Ukumbi wa Kongamano hilo, kushoto kwake ni Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema pamoja na washiriki wengine wa Kongamano hilo lililofanyika Nchini China
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo mara baada ya majadiliano kuhusu uwezekano wa kupata Fursa za Miradi kwenye Hifadhi Hai katika Kongamano la Dunia la Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai lililofanyika jijini Hangzhou nchini China. Kulia kwake ni Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA KIKANDA NCHINI UGANDA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Warsha ya Kikanda Jijini Kampala (EAC) inayohusu masuala ya upangaji wa maeneo ya ufugaji samaki katika ziwa Victoria.

Akiripoti kutokea Kampala Meneja kutoka NEMC Bw.Jarome Kayombo amesema warsa hiyo imelenga kuainisha vigezo vitalavyotumika kwa nchi zote tatu katika kupanga maeneo ya ufugaji, kutenga maeneo, kusimamia mazingira na usalama w Samaki.

Wajumbe walioshiriki kutoka Tanzania ni pamoja na Wizara ya Mifugo, NEMC, Bonde ziwa Victoria, Jumuia ya wafugaji Samaki, Umoja wa wavuvi, Vyuo vikuu pamoja na Tafiri.

Ujumbe ulioambatana na timu hiyo katika warsha umehusisha Uganda, Kenya, Tanzania, Burundi na Rwanda.

Meneja kutoka NEMC Bw. Jarome Kayombo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Warsha ya Kikanda Jijini Kampala (EAC) inayohusu masuala ya upangaji wa maeneo ya ufugaji samaki katika ziwa Victoria.

NEMC YATEMBELEA KIWANDA NCHINI NORWAY KUJIFUNZA UZALISHAJI SARUJI ISIYOZALISHA HEWA UKAA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati, PURA na TANESCO, wametembelea Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway, kinachoendeshwa na kampuni ya Norcem chini ya Heidelberg Materials, ambacho ni kiwanda cha kwanza duniani cha saruji kuendesha kituo kamili cha kunasa na kuhifadhi hewa ya ukaa (CCS). Sekta ya saruji ni ngumu kupunguza hewa ya ukaa kwa sababu malighafi yake kuu (chokaa), huzalisha kaboni dioksaidi wakati wa mchakato.

Baadhi ya Wataalamu wa Mazingira wa NEMC na Wataalamu wa Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway wakiwa katika picha ya pamoja 

Kiwanda hiki kinatumia teknolojia ya kunasa dioksidi kaboni kwa njia ya amini (amine absorption) ambapo gesi ya ukaa hutenganishwa kutoka kwenye moshi wa mitambo, kisha hubanwa (compressed) na kubadilishwa kuwa kimiminika ili kusafirishwa. Ukaa ulionaswa unasafirishwa kupitia mtandao wa hifadhi wa Northern Lights. Baada ya kubadilishwa kuwa kimiminika, husafirishwa kwa meli hadi kituo cha nchi kavu kisha huingizwa kwenye tabaka za miamba ya ardhini chini ya Bahari ya Kaskazini. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Longship wa Norway unaolenga kusaidia viwanda kupunguza hewa chafu ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Mradi huu wenye thamani ya takriban Euro milioni 400 unategemea ushirikiano wa karibu na msaada mkubwa wa kifedha wa serikali (takriban 75%) kutokana na gharama zake kubwa za kiufundi. Pia mradi huu umewezesha kutengenezwa kwa bidhaa mpya za saruji zenye alama ya “evoZero”, zinazouzwa kama saruji yenye uzalishaji usio na hewa ya ukaa kwa sababu ukaa wake unanaswa na kuhifadhiwa. Mafunzo na uzoefu unaopatikana hapa yanatarajiwa kusaidia katika utekelezaji wa miradi mingine ya CCS Duniani kote.

Kwa ujumla, kituo cha CCS cha Brevik kinaonyesha kuwa inawezekana kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa katika sekta ya saruji. Ingawa bado kuna changamoto za gharama na matumizi makubwa ya nishati, mradi huu ni hatua kubwa ya kihistoria katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ni mfano bora kwa viwanda vingine vizito vinavyolenga kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ya ukaa.

WAHANDISI WA NEMC WASHIRIKI MAADHIMISHO YA 22 YA SIKU YA WAHANDISI NCHINI (22ND AED 2025)

Wahandisi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wanashiriki Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi nchini (AED 2025) yanayofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 - 26 Septemba, 2025 chini ya kauli mbiu isemayo "Kufanikisha Dira ya 2025 na Kusonga Mbele kuelekea Dira ya 2050: Nafasi ya Wahandisi."

Tukio hili limewaleta pamoja wahandisi zaidi ya 4,000, watunga sera, na wadau mbalimbali kujadili masuala muhimu ikiwemo maadili katika uhandisi, mabadiliko ya kidijitali, miundombinu ya kijani, nishati, maji, kilimo, ushindani wa viwanda, na maendeleo endelevu.

Kupitia ushiriki huu, wahandisi wa NEMC wanaendelea kuimarisha nafasi yao katika kuunganisha ubunifu wa uhandisi na uwajibikaji katika kusimamia uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha kwamba safari ya Tanzania kuelekea Dira ya 2050 inabaki endelevu, jumuishi, na yenye ustahimilivu.


Wahandisi wa Mazingira (NEMC) wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam  wakati wa Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi nchini 

NEMC YASHIRIKI KONGAMANO LA UNESCO LA PROGRAMU YA BINADAMU NA HIFADHI HAI CHINA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Kongamano la Dunia la Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai lililofanyika Jijini Hangzhou nchini China kuanzia tarehe 22-25 Septemba 2025.

Kwa upande wa NEMC Kongamano hilo limehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi pamoja na Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema.

Wawakilishi wengine kutoka Tanzania katika kongamano hilo ni kutoka TANAPA

Kongamano hilo limelenga Kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa, kupata maarifa na teknolojia mpya katika kusimamia na kuhifadhi Mazingira nchini, ni fursa katika uendelevu wa Hifadhi za Taifa, fursa za Kutangaza vivutio vya kitalii, kuimarisha Ushirikiano na Jamii, kuitangaza Tanzania kimataifa, kuvutia wawekezaji na kusaidia kufikia malengo ya Maendeleo nchini.


Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kushoto) katika Ukumbi wa Kongamano hilo, kushoto kwake ni Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema pamoja na washiriki wengine wa Kongamano hilo lililofanyika Nchini China

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Tafiti za Mazingira(NEMC) Dkt. Rose Sallema na mshiriki mwingine wa Kongamano hilo

Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema (wa katikati) na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.


NEMC NA TANAPA WAADHIMISHA SIKU YA FARU DUNIANI KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI- KILIMANJARO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na TANAPA wameadhimisha Siku ya Faru Duniani ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Same mkoani Kilimanjaro Septemba 22,2025.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Afisa Mazingira Mwandamizi Bw. Francis Nyamhanga amezungumzia kuhusu umuhimu wa Faru kwenye mfumo wa Ikolojia.

"Kwenye mfumo wa Ikolojia Faru husaidia kufungua njia kwa kuvunja miti kwa ajili ya Wanyama wengine wadogo kuweza kupata malisho lakini pia hula mbegu za mimea mbalimbali hivyo kupitia kinyesi chao husaidia kusambaza mbegu katika mifumo Ikolojia na kinyesi hicho pia hurutubisha mifumo ikolojia bila kusahau wanachangia kukuza pato la Taifa kwani Faru ni kivutio cha utalii" amesema Bw. Francis.

 Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo na Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Bw. Francis Nyamhanga wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomanzi Mkoani Kilimanjaro katika Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani

Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo ameeleza namna wanavyowafikia Jamii kwa kutoa elimu ya Uhifadhi wa Faru.

"Hifadhi Ina programu maalumu inayofahamika kama Rafiki wa Faru ambayo inafikia Jamii kwa kuipa elimu ya jinsi ya Faru hawa walivyotoweka, walivyorejeshwa na jinsi wanavyolindwa na kuzalishwa katika Hifadhi hii. Hadi sasa tumefikia shule 120 na kuwafikia walimu na wanafunzi takribani 3,600 toka Julai 2022" amesema Mhifadhi Lyimo.

Katika kuadhimisha Siku hii pia wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamefika katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kujifunza namna Uhifadhi wa Faru unavyofanyika. Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani hufanyika mnamo Septemba 22 kila mwaka kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusiana na Uhifadhi wa Faru na kuwalinda dhidi ya ujangili.






NEMC YAADHIMISHA SIKU YA USAFI DUNIANI KWA KUFANYA USAFI HOSPITAL YA MWANANYAMALA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani tarehe 20 Septemba ya kila mwaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, akiwemo DEPO, limefanya usafi Hospitali ya Mwananyamala na maeneo mengine nchi nzima ambapo Kanda 13 zipo zikitoa huduma za Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira.

Zoezi hilo limehusisha watumishi wa NEMC, wawakilishi kutoka DEPO, pamoja na baadhi ya wananchi wa maeneo ya jirani, ambapo usafi mkubwa umefanyika katika mazingira ya hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuondoa taka, kufagia, na kusafisha mitaro ya maji taka.

Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, tarehe 20 Septemba.

Akizungumza katika zoezi hilo, Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwa na mazingira safi, salama na endelevu kwa afya na maendeleo ya Taifa.

"Siku hii si ya kusherehekea tu, bali ni ya kutafakari na kuchukua hatua. Mazingira safi ni msingi wa afya bora, ukiangalia taka zilizookotwa hapa nyingi ni za majumbani, kunamifuko ya plastiki, chupa, mabaki ya vyakula ambazo zingetakiwa kutenganishwa kutokea nyumbani. Tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema.

Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya zoezi hilo

Kwa upande wake, mwakilishi wa DEPO, Bw. Humphrey Milinga alieleza kuwa ushirikiano kati ya mashirika ya mazingira na Taasisi za afya ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inapata huduma katika mazingira rafiki na salama.

"Tumeona ni vyema kufanya usafi hospitalini kwani ni maeneo ya kuhudumia afya, na mazingira yake yanapokuwa safi, yanasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa," aliongeza.

Katika maadhimisho hayo, kanda mbalimbali za NEMC pia zilitekeleza shughuli za usafi katika maeneo yao husika, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya usafi inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jamii nzima katika kulinda mazingira.

Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, 20 Sepemba.

Siku ya Usafi Duniani huadhimishwa duniani kote kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira, kuondoa taka, na kuelimisha jamii juu ya athari za uchafuzi wa mazingira.

NEMC imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye mazingira safi na salama kwa wote.

Picha ya pamoja ya watumishi wa NEMC, DEPO, Hospitali ya Mwananyamala na wakazi wa Mwananyamala mara baada ya zoezi la Usafi wa Mazingira ya Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu katika kuadhimisha siku ya Usafi Duniani.

NEMC YAINGIA MTAANI KIDIGITALI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam  linaendesha zoezi maalumu la Ukaguzi wa Mazingira kwa Miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mfumo maalumu wa kidigitali uitwao 'Mazingira App'.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti amesema zoezi hilo litadumu kwa wiki nne na litahusisha kaguzi za Mazingira kwenye miradi ya maendeleo hususani kuangalia uzingatiaji wa matakwa ya Usimamizi wa Mazingira kama vile usimamizi wa taka, matumizi sahihi ya ardhi pamoja na  uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti (wa kwanza kushoto) akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu zoezi maalumu la Ukaguzi wa Mazingira kwa Miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mfumo maalumu wa kidigitali uitwao 'Mazingira App'.

Ameongeza kwa kutumia mfumo wa Mazingira App pia utawawezesha kuchunguza uzingatiaji wa Sheria zinazohusu afya ya jamii, usalama wa kazi na mipango miji  ambazo kwa kutokutekelezwa kwake huchangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi au uharibifu wa mazingira.

Aidha Bw. Jamal Baruti amesema ushirikiano na uongozi wa Jiji la Dar es salaam umelenga kuongeza uelewa na ufanisi kwa maafisa mazingira kuhusu Usimamizi hafifu wa taka ngumu, changamoto ya taka za plastiki, uharibifu wa Mazingira kutokana na uchimbaji holela wa kwenye mito na mabonde na matumizi holela ya ardhi kinyume na taratibu za mipangomiji.

Kwa upande wake Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki (NEMC) Bi. Glory Kombe alipozungumza amewataka Viongozi wa Halmashauri na Serikali za mitaa kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi hili ili kufikia tija tarajiwa kwa maendeleo endelevu ya Mazingira nchini.

Kadhalika Meneja Glory Kombe amefafanua  kuwa jukumu la Halmashauri na Mamlaka za Serikali za mitaa ni kuhakikisha Miradi ya maendeleo inazingatia taratibu za Mazingira ikiwemo ufanyikaji wa Tathmini ya Mazingira na Jamii kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Mazingira na Kanuni zake na kusimamia usafi wa Mazingira kwa ujumla pamoja na kuwataka maofisa Mazingira na Kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.

Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki Bi. Glory Kombe (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huo
Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC)Bw. Hamadi Taimuru (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huo

 NEMC imeanzisha mfumo huo wa Mazingira app' ambao ni wa kidigitali ili kurahisisha na kuongeza  ufanisi katika ukusanyaji na uhifadhi wa Taarifa za Miradi pamoja na usajili wa Miradi mipya ambapo zitachangia Baraza na Serikali kupanga na kusimamia Miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.



NEMC YAKAGUA MGODI WA 'URANIUM' MKOANI RUVUMA UNAOTARAJIWA KUANZA 2026

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilifika na kukagua Mgodi wa madini aina ya Uranium uliopo katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambao ulikuwa katika Uchimbaji mdogo wa majaribio huku Uchimbaji mkubwa ukitarajiwa kuanza mwaka 2026.

NEMC ilifika na kufanya Ukaguzi katika Mgodi huo na kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha shughuli za Uchimbaji katika Mgodi huo haziathiri Mazingira, Viumbe hai na wakazi wa jirani na Mgodi huo ikiwa ni agizo la Serikali.

Awali NEMC ilianza kwa kutoa elimu ya Mazingira na Afya kwa wakazi wa vijiji vilivyo karibu na Mgodi huo ili kuwajengea uelewa kuhusiana na madini ya 'Uranium' jinsi yanavyoweza kuhatarisha afya na Mazingira ikiwa hayata chakatwa na kudhibitiwa kwa umakini.

Akizungumza katika Ukaguzi huo Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Bw. Jamal Baruti alisema NEMC ilifika katika Mgodi huo kufanya Ukaguzi ili kutathmini ikiwa wawekezaji katika Mgodi huo wamekidhi na kuzingatia miondombinu ya Mazingira ambayo haita haribu Mazingira, kuhatarisha usalama wa wakazi na wafanyakazi katika Mgodi huo kabla Uchimbaji mkubwa haujaanza.

Timu ya wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Kampuni ya Uchimbaji ya MANTRA wakikagua moja ya mlima wenye madini ya  'Urunium' wakati wa ukaguzi wa Mgodi huo. Wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti.

Aidha Bw. Baruti alieleza kuwa Mradi wa Mgodi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani elfu 27 kwa siku na utakuwa ni Mradi mkubwa wa Uchimbaji madini nchini ukilinganisha na Miradi mingine nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa Tanzania  itakuwa nchi ya nne ya uzalishaji wa madini ya 'Uranium' Duniani huku akiwasisitiza wawekezaji na wananchi kuzingatia uhifadhi Mazingira na si tu kuangalia manufaa ya Mgodi huo.

Meneja wa Kampuni ya MANTRA Bw. Beria Vorster akitoa maelezo kwa wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC wakati wa ukaguzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya 'Urunium' ikiwa ni sehemu ya Ukaguzi wa Mgodi huo.

Kwa upande wake Meneja Kanda ya Kusini (NEMC) Bw. Boniface Guni alisema ziara hiyo iliwasaidia NEMC kupata picha ya Mradi huo ambayo itawasaidia kusimamia Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na jamii ipasavyo.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buchushu Kijiji cha Iguseka Bw. Omary Rashid aliishukuru NEMC kwa kuwapatia elimu hiyo adhimu ya Mazingira wakazi wa vijiji hivyo ambayo ni muhimu katika utunzaji wa Mazingira na Afya ya binadamu.

Timu ya wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Kampuni ya Uchimbaji ya MANTRA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ukaguzi wa Mgodi wa madini ya 'Urunium' katika eneo la Mto Mkuju Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma. Wa katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti na kushoto kwake ni Meneja wa Mradi Bw. Beria Vorster

RUVUMA YAFIKIWA ELIMU YA MAZINGIRA- MADINI YA URANIUM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitoa elimu ya kimazingira na afya kwa vijiji viwili vya Mtonya na Mandela-Likuyu katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kufuatia Mradi wa Uchimbaji wa Madini aina ya 'Uranium'  ulitarajiwa kuanza katika mgodi ulio karibu na vijiji hivyo.

Elimu hiyo ilitolewa kwa wananchi kuanzia 8-9 Septemba, 2025 kwa vijiji hivyo huku ikifuatiwa na ukaguzi uliofanyika katika mgodi huo ambapo ilikuwa hatua ya awali ya kuelimisha jamii na wawekezaji kabla ya Mradi huo kuanza ambapo  ni maagizo yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha jamii inatambua uwepo wa Mradi huo na kuhakikisha  jamii haiathiriki na Mradi huo.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti akizungumza wakati wa utoaji wa elimu ya ya Mazingira na Afya kwa wanakijiji wa Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Meneja Kanda ya Kusini NEMC Bw. Boniface Guni akiwasilisha mada kwa wanakijiji wa Mandela-Likuyu Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wakati wa utoaji wa elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Meneja Kanda ya Kusini NEMC Bw. Boniface Guni akiwasilisha mada kwa wanakijiji wa Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wakati wa utoaji wa elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Akizungumza katika utoaji wa elimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti aliutaka Uongozi wa vijiji hivyo kutumia Kamati za Mazingira na kushirikiana na Serikali kuendelea kuelimisha jamii juu ya maswala ya Mazingira na Afya ya jamii yanayoweza kusababishwa na Mradi huo.

Kwa upande wake, Meneja Kanda ya Kusini (NEMC) Bw. Boniface Guni aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuchangamkia fursa za ajira katika Mradi huo huku wakizingatia ulinzi wa Afya zao na Mazingira.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti alisema NEMC itaendelea na ufuatiliaji wa maswala ya kimazingira kwa kushirikiana na Taasisi nyingine huku akiitaka Kampuni ya Mantra TZ LTD ya Uchimbaji katika mgodi huo kutambua haki za wakazi wa vijiji hivyo na kuchangia shughuli za maendeleo ya wakazi wa vijiji hivyo kama manufaa ya Mradi huo.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti (wa tatu kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanakijiji na Viongozi wa Kijiji cha Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma mara baada ya kuwapatia elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

NEMC YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI KUSINI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji Kusini (Kusini International Trade Fair and Festival) yanayofanyika kuanzia tarehe 14-21, Septemba, 2025 katika eneo la fukwe ya Matema Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya.

Maonesho hayo yamelenga kutangaza fursa za kibiashara zilizopo katika mikoa ya Kusini ambapo NEMC inatumia fursa hiyo kutoa elimu ya Mazingira.


Maafisa Mazingira wa NEMC Kanda ya Kusini wakitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda lao katika maonesho hayo.

DKT. SERERA AVUTIWA NA USHIRIKI WA NEMC KWENYE MAONESHO YA BIASHARA YA KIMATAIFA BARANI AFRIKA (IATE)

Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa namna ambavyo linatoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Barani Afrika yanayotambulika kama Intra African Trade Fair (IATF) yanayoendelea jijini Algiers nchini Algeria kuanzia Septemba 4-10, 2025.

Dkt. Serera ambaye ni Mkuu wa msafara wa Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Maonesho hayo, ametoa pongezi hizo alipofika Banda la Tanzania akiambatana na mwenyeji wake ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman S. Njalikai.

Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera akizungumza na Mhandisi Mwandamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Peres Ntiginya wakati alipotembelea Banda la Tanzania katika maonesho hayo

"Uchumi tunaoutaja ni Uchumi wa Viwanda, lakini Viwanda tunavyohitaji ni viwanda vinavyozingatia Uhifadhi wa Mazingira, hivyo basi NEMC kwa kuja hapa wanawaambia wawekezaji waje lakini yapo ya kuzingatia kuhusu Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira" amesema Dkt. Serera.

"NEMC inalo jukumu la kuendelea kutoa elimu na nilichopenda zaidi ni kwamba hakuna urasimu, nimeona hapa taarifa zote unaweza kuzisoma na kuzipata kupitia "QR Code" kabla hata ya kuja kuwekeza Tanzania, Na hapa niwapongeze sana NEMC kwa namna mnavyofanya kazi vizuri na muendelee hivyo kwani Mazingira ni uhai ni lazima tuyatunze ili yatutunze" Amesisitiza Dkt. Serera.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Imani S. Njalikai amezitaka Taasisi zinazoshiriki Maonesho hayo kuitumia fursa hii vizuri hasa katika maeneo ambayo Algeria inafanya vizuri kwenye sekta ya nishati ambayo ni pamoja na gesi, mafuta, mbolea na sekta ya madawa (pharmaceutical) ambayo ni pamoja na mafunzo kwenye maeneo hayo.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Barani Afrika yanayotambulika kama Intra African Trade Fair (IATF) yaliyofanyika jijini Algiers nchini Algeria kuanzia Septemba 4-10, 2025.

NEMC ikiwa ni moja ya Taasisi inayoshiriki Maonesho hayo ikiwakilishwa na Mhandisi Mkuu, Peres Ntinginya na Afisa Uhusiano na Mawasiliano, Bw. Tajiri Kihemba. Taasisi nyingine zinazoshiriki ni pamoja na TANTRADE ambao ni waratibu kwa upande wa Tanzania, TMDA, FCC, TISEZA, PURA, TFS, ZIPA.

NEMC YASHIRIKIANA NA ASASI ZA KIRAIA KUSAFISHA FUKWE YA COCO, ΝΙΚΑΤΙΚΑ KUTΕΚELEΖΑ ΚΑΜΡENI YA ΝΕΜC USAFI KAMPENI'

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, Asasi za kiraia na wakazi wa karibu na maeneo ya fukwe ya Coco leo 6 Septemba, 2025 wamefanya usafi wa fukwe ya Coco ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Kampeni ya 'NEMC Usafi Kampeni' iliyozinduliwa rasmi 4 Septemba, 2025.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mhandisi wa Mazingira (NEMC) Bw. Joshua Muro amesema NEMC ipo tayari kushirikiana na jamii pamoja na Asasi za kiraia katika kutekeleza Kampeni hiyo ya 'NEMC Usafi Kampeni' yenye lengo la kuhamasisha jamii kusafisha na kuhifadhi Mazingira, Pia ameitaka jamii kubadili mtazamo juu ya jukumu la usafi wa Mazingira na kufafanua kuwa ni jukumu la kila mmoja kufanya usafi wa Mazingira yanayomzunguka.

Baadhi ya watumishi wa NEMC na DEPO wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya zoezi la usafi katika Fukwe ya Coco

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Asasi ya DEPO, Ndugu. Humphrey Milinga amesema lengo kubwa la zoezi hilo ni kuhamasisha jamii katika ngazi ya familia kusafisha Mazingira na kujumuika katika vikundi vya usafishaji Mazingira zikiwemo Fukwe.

Washiriki wengine walio jumuika katika zoezi hilo ni Africraft, MBC, WWF, TIA, TESCAR na Bethlehem Parish.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Mazingira na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Asasi za kiraia pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa na safi na salama kwa ustawi wa Afya na Mazingira.

Baadhi ya wakazi wa maeneo ya jirani na Fukwe ya Coco na baadhi ya watumishi wa NEMC kisafisha Fukwe hiyo


NEMC YAJA NA USAFI KAMPENI 2025

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezindua kampeni mpya ya usafi iitwayo "NEMC Usafi Kampeni' 2025" yenye lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika usafi wa mazingira na kuhakikisha nchi inakuwa safi, salama na yenye afya kwa wote.

Kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, mamlaka za mikoa na Halmashauri, Taasisi binafsi, Asasi zisizo za kiserikali na wananchi, inalenga kuibua mabadiliko ya tabia na kukuza uwajibikaji wa pamoja katika kudhibiti ongezeko la uchafuzi wa mazingira, hasa taka ngumu na plastiki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezajinwa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu alisema kwa sasa Tanzania inazalisha takriban tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka kwa mwaka, huku wastani wa uzalishaji taka kwa mtu mmoja ukiwa kati ya kilo 0.66 hadi 0.95 kwa siku. Hali hii inahitaji jitihada za dhati kutoka kwa kila mtanzania.

"Kampeni hii inalenga kuondoa dhana kuwa usafi ni jukumu la serikali pekee. Kila mtu anapaswa kushiriki, kwa kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inamtaka kila mtu kuwa mdau na mlinzi wa mazingira," alisema Baruti.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti akizungumza na Vyombo vya habari katika Uzinduzi wa Kampeni hiyo

Aliongeza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo imeweka hifadhi ya mazingira kuwa moja ya mihimili ya maendeleo endelevu. Kupitia kampeni hii, taka zitatazamwa kama fursa ya ajira kupitia miradi ya kijani, vijana na wanawake watawezeshwa kupitia mafunzo ya ujasiriamali wa mazingira, huku upandaji miti ukihamasishwa kwa nguvu zote.

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika chini ya kampeni hiyo ni pamoja na operesheni za usafi, mafunzo ya elimu ya mazingira, mashindano ya usafi kwa shule na kata, uanzishaji wa bustani za kijani, maonesho ya bidhaa rafiki kwa mazingira, pamoja na uanzishwaji wa klabu za mazingira katika shule zote za msingi na sekondari ifikapo Juni 2026.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezajinwa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti akizungumza na Vyombo vya habari katika Uzinduzi wa Kampeni hiyo

Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamad Taimuru (kushoto) akielezea jambo wakati  wa uzinduzi wa "NEMC Usafi Kampeni"..

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...