Nyumbani

NEMC YAKUTANA NA TAASISI ZA SERIKALI NA WADAU WA SEKTA YA MADINI GEITA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya mkutano na wadau wa mazingira tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukumbusha wadau kuhusu haki na wajibu wao katika kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake. Katika mkutano huo, viongozi wa NEMC waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuimarisha uelewa wa utekelezaji sahihi wa sheria hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira.


Aidha, wawekezaji walisisitizwa umuhimu wa kufanya usajili na kukamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao. Hatua hii inalenga kulinda mazingira, afya za binadamu na viumbe hai wengine, pamoja na kuepusha hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya miradi isiyozingatia taratibu.


Kwa upande mwingine, taasisi za serikali zilihimizwa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za mazingira. NEMC imeeleza kuwa itaendelea kuandaa mikutano kama hii katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji kuelekea maendeleo endelevu ya taifa.


Taasisi za serikali zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Halmashauri za Geita, Kahama na Shinyanga, Tume ya Madini, Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

TAKA SI UCHAFU TENA, TAKA NI FURSA!


📌 Waziri Masauni aipongeza NEMC kwa kubadilisha mitazamo ya watu juu ya Taka

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, ameipongeza NEMC kwa kushirikiana na wadau wa mazingira katika juhudi za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu taka na kuzigeuza kuwa fursa yenye manufaa ya kiuchumi na kimazingira.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka Duniani yaliyofanyika leo, Machi 30, 2026, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mhe. Masauni amesisitiza umuhimu wa kuendeleza dhana ya kupunguza, kutumia tena na kurejeleza taka (Reduce, Reuse, Recycle), sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “kupunguza taka katika sekta ya chakula.”

"Taka siyo uchafu bali ni fursa; tukizisimamia vizuri tunaweza kuzigeuza kuwa rasilimali yenye thamani kwa maendeleo endelevu.” Amesema Waziri Masauni.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesisitiza kuendelea kwa utoaji wa elimu ya mazingira hususan shuleni kuanzia ngazi ya msingi, pamoja na kuimarisha mafunzo kwa makampuni ya ukusanyaji taka kwa kushirikiana na NEMC ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa jamii ili kuongeza uelewa juu ya usimamizi bora wa taka na kuchochea ushiriki wa wananchi katika kulinda mazingira.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua thamani ya taka na kuzitumia kama rasilimali kwa maendeleo endelevu, huku yakiwakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira.













𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗢𝗡𝗚𝗢𝗭𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗔𝗡𝗢- 𝗪𝗔𝗥𝗦𝗛𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗞𝗔𝗡𝗗𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗜 𝗬𝗔𝗞𝗘 𝗡𝗔 𝗖𝗦𝗘 𝗡𝗔 𝗜𝗡𝗗𝗜𝗔



 𝗡𝗶 𝗞𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗙𝘂𝗿𝘀𝗮 𝘇𝗶𝗹𝗶𝘇𝗼𝗽𝗼 𝗸𝘄𝗲𝗻𝘆𝗲 𝗨𝘀𝗶𝗺𝗮𝗺𝗶𝘇𝗶 𝘄𝗮 𝘁𝗮𝗸𝗮 𝘇𝗮 𝗠𝗮𝘁𝗮𝗶𝗿𝗶 𝗖𝗵𝗮𝗸𝗮𝘃𝘂

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Machi 25, 2026, limeendelea kuongoza majadiliano katika siku ya pili ya warsha ya Kikanda kuchochea fursa mpya katika Usimamizi wa taka za matairi chakavu ambapo mawasilisho ya kanuni za Usimamizi wa matairi chakavu (End-of-Life Tyres – ELTs) katika nchi zinazotekeleza mfumo wa Extended Producer Responsibility (EPR) yalifanyika.

Aidha, wasilisho la kitaalamu kutoka kituo cha Afrika Kusini cha kukuza uzalishaji wa kijani kuhusu umuhimu wa usimamizi wa matairi chakavu katika kulinda mazingira, kuchochea uchumi wa kijani na kuunda ajira, huku washiriki kutoka Ghana wakishirikisha uzoefu wa matumizi mbadala ya matairi chakavu na mbinu za kuwaunganisha wakusanyaji wadogo katika mfumo rasmi.

Kadhalika, mwakilishi kutoka Much Asphalt - Afrika Kusini aliwasilisha kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa zinazotumia matairi chakavu katika ujenzi wa barabara kama njia ya kuongeza thamani ya taka na kuboresha uimara wa barabara.

Kupitia warsha hiyo, NEMC imeongeza uelewa wa kuhusu mbinu bora za kuthibiti taka zitokanazo na matairi chakavu na kukuza uchumi rejeleshi.

MAAFISA HABARI NA WADAU WA ELIMU KWA UMMA WASISITIZWA KUWAUNGANISHA WANANCHI



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali pamoja na wadau wengine wa Elimu kwa Umma kutumia nafasi zao kuwaunganisha Watanzania kwa kutoa taarifa zenye kuleta tija kwa jamii kwa kuzingatia weledi, ujuzi na ubunifu.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ametoa wito huo alipokuwa akifungua Mkutano wa 110 wa Wadau wa Elimu kwa Umma unaofanyika jijini Arusha kuanzia Machi 23 hadi 27, 2025 katika Ukumbi wa PAPU akiwa ndiye Mgeni Rasmi ambapo amewataka wadau hao wa elimu kwa Umma ambao asilimia kubwa ni Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali kuhakikisha wanaongeza ubunifu katika kufikisha taarifa zenye kuwaunganisha Watanzania.

"Tumieni nafasi zenu kuunganisha Watanzania na kupitia mada zinazofundishwa ni imani yangu kwamba zitaongeza weledi na ujuzi, hivyo tumieni vizuri kuongeza ubunifu katika kuwaeleza wananchi kuhusu mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali" Amesema Dkt. Mwigulu.

Pia Dkt. Mwigulu amesisitiza Wadau hao wa elimu kwa Umma kujenga utamaduni wa kufanya Tafiti kupata taarifa sahihi kabla ya kupeleka kwa wananchi huku akiwataka wadau hao kuhakikisha wanatoa taarifa wakiwa na uelewa juu ya taarifa hizo wanazozitoa.

"Ni lazima msome na kuelewa kile mnachokipeleka kwa wananchi, huku mkihakikisha kwamba mnalinda Taswira za Taasisi zenu" Amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ni moja kati ya Taasisi zinazoshiriki Mkutano huo kwa kuwakilishwa na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wake, Bw. Tajiri Kihemba ikizingatiwa kwamba NEMC ni kati ya wadau Muhimu wa masuala ya utoaji wa elimu kwa Umma katika eneo la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.

Mkutano huu umeandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa wadau wa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kutimiza jukumu hilo muhimu ili kufanikisha kufikisha taarifa kwa Watanzania na wadau wengine wa maendeleo nchini.

NEMC NA UDSM WAANDAA KONGAMANO LA UZINDUZI WA MTAMBO WA NISHATI SAFI YA HAIDROJENI

 Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi Binafsi ya Bora Women Go Green limeandaa Kongamano la uzinduzi wa mtambo wa Nishati safi ya kupikia aina ya haidrojeni likiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini lililofanyika leo Machi 25, 2026 katika Ukumbi wa Nkurumah Hall wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Akizungumza katika uzinduzi wa mtambo huo, Mgeni rasmi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Festo Dugange amesema uzinduzi wa mtambo huo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Aidha Dkt. Dungage amesisitiza kuwa ili kukabiliana na changamoto na athari za mazingira na zile za mabadiliko ya tabianchi, ni lazima kuongeza jitihada za Utunzaji na Usimamizi wa mazingira, kuwekeza kwenye vyanzo vya nishati mbadala na kuwa na mifumo ya kusaidia kustahimili mabadiliko ya tabianchi.


Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030, akitaja vyanzo kama umeme, bayogesi, haidrojeni, gesi asilia, nishati ya jua, majiko banifu na mkaa mbadala kuwa ni suluhisho la kudumu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema uzinduzi huo sio tu ishara ya maendeleo ya teknolojia, bali pia ni uwekezaji katika ubunifu na uwezo wa vijana wa Kitanzania.


Ameongeza kuwa matumizi ya mtambo huo yana uwezo wa kubadilisha maisha ya jamii kwa kupunguza gharama, kulinda afya dhidi ya moshi wa kupikia, na kuhifadhi mazingira, huku akizipongeza taasisi zote zilizohusika kufanikisha kongamano hilo.









Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la kimataifa la WaterAid-Tanzania, limefanya ziara ya mafunzo nchini Rwanda. Mafunzo haya yameandaliwa na kutekelezwa na WaterAid-Rwanda, na yamefanyika katika Ofisi za shirika hilo.

Lengo kuu la mafunzo haya ni kujifunza namna WaterAid-Rwanda inavyotekeleza miradi ya maji, hususan katika eneo la Bugesera, ikiwa ni pamoja na mbinu za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira.

Ziara hii ya mafunzo imehudhuriwa na viongozi na wataalamu mbalimbali, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mkurugenzi Msaidizi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira, Afisa Tawala wa Mkoa wa Manyara, pamoja na maafisa wengine kutoka serikalini na WaterAid

NEMC, CSE WAANDAA WARSHA YA KIKANDA KUCHOCHEA FURSA MPYA KATIKA USIMAMIZI WA TAKA ZA MATAIRI CHAKAVU

 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Kituo cha Sayansi na Mazingira - India (CSE) wameandaa warsha ya kikanda inayolenga kujadili changamoto na fursa zitokanazo na ongezeko la taka za matairi chakavu.

 Warsha hiyo imewakutanisha washiriki kutoka mamlaka za usimamizi wa mazingira na wadau mbalimbali kutoka nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Ghana na Nigeria. Mkutano huu umefanyika katika Hoteli ya Four Points by Sheraton na New Africa Hotel jijini Dar es Salaam tarehe 23 na 24 Machi 2026.

Katika warsha hiyo, mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwemo miundo ya kisheria na kikanuni, teknolojia za kuongeza thamani ya taka za matairi, pamoja na matumizi ya masoko katika kukuza dhana ya uchumi rejeleshi. Lengo kuu ni kubadilishana uzoefu na kubuni mbinu mbadala zitakazosaidia kupunguza athari za kimazingira huku zikichangia maendeleo endelevu ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika.





𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa ...